Wakuu wa fedha duniani wakutana nchini Mauritania.
1 Agosti 2008Mawaziri wa fedha wa mataifa ya Afrika na magavana wa benki kuu za mataifa hayo wamekutana na wenzao wa taasisi za fedha za kimataifa za IMF na benki kuu ya dunia leo Ijumaa wakiwa na matumaini ya kuweka miongozo juu ya kushughulikia uwekezaji mpya katika bara hilo, mingi ikiwa ni kutoka China.
China , Brazil na India zimekuwa zikifunga mikataba ya mikopo na miundo mbinu katika bara la Afrika , ikiwa mara nyingi ni kwa kupata mafuta, madini ya chuma pamoja na vyanzo vingine wanavyohitaji kuimarisha uchumi wao unaokua kwa kasi.
Wakopeshaji wakuu wa jadi kama shirika la fedha la kimataifa IMF na benki kuu wanahofu kuwa mataifa ya Afrika ambayo yanafaidika hivi sasa na nafuu kutokana na kufutiwa madeni huenda yakajilimbikizia madeni mengine ambayo watakujajikuta wanashindwa kuyalipa, hususan iwapo bidhaa wanazouza zitamalizika.
Tumeamua kutenga siku ili kulizungumzia suala hili la vyanzo ambavyo si vya kawaida vya fedha , ambavyo ni China, India, Brazil pamoja na mashirika yanayotoa mikopo mbali na mashirika ya kawaida ya IMF na benki kuu ya dunia, ili kufafanua jinsi IMF na benki kuu ya dunia zinavyokubali shauku ya vyanzo hivi vipya ya kutoa fedha kwa mataifa ya Afrika, amesema Ousmane Kane, gavana wa bnki kuu ya Mauritania na mwakilishi wa kundi la mataifa ya Afrika katika benki kuu ya dunia na IMF.
Mkutano huo wa kundi la mataifa ya Afrika nchini Mauritania, unaokutanisha magavana wa benki kuu na mawaziri wa fedha kutoka katika mataifa masikini ya bara hilo, watakuwa na kikao ili kukubaliana msimamo wa pamoja juu ya wawekezaji wapya, kwa kiasi kikubwa wakitumika kama wakopeshaji mbadala wa wale wa zamani.
Mbali ya mikopo, mikataba na China mara nyingi inahusisha wafanyakazi wa China wanaojenga mabarabara pamoja na miradi mingine ya miundo mbinu, wakati maliasili zinakwenda upande mmoja na kiasi ni kikubwa mno.
Maafisa wa IMF wanasema kuwa wanahitaji kuchunguza athari za mikopo za mkataba wa dola bilioni 9 wa madini na miundo mbinu kati ya China na jamhuri ya kidemokrasi ya China kabla ya kuamua iwapo DRC inastahili kuingia katika mpango wa IMF na hatimaye kuingia katika mpango wa nafuu ya madeni.
Wanasiasa wa upinzani na makundi ya kupambana na rushwa nchini Niger wamekosoa ukosefu wa uwazi katika mikataba kati ya serikali na kampuni la mafuta la China CNCP ambao unaweza kuwa na thamani ya dola bilioni 5 kwa moja kati ya nchi masikini sana duniani.
Manufaa kutoka kwa wakopeshaji wapya ni kwamba wanaangalia mahitaji ya Afrika , ambayo ni miundo mbinu, wakati wakopeshaji wa zamani wanalenga tu katika elimu, amesema afisa mmoja kutoka taasisi ya fedha aliyehudhuria katika mkutano huo.
Mjumbe mwingine akahitimisha kwa kusema utake usitake China ni sehemu kubwa ya Afrika hivi sasa.
Wakati huo huo mkurugenzi mtendaji wa IMF Dominique Strauss Kahn amesema katika mkutano huo leo kuwa mataifa ya Afrika ambayo yanajaribu kusaidia wananchi wake kupambana na bei za juu za chakula , walenge katika hatua za kusaidia familia masikini na kuepuka matumizi mabaya. Amewaambia mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu za mataifa ya Afrika katika mkutano huo nchini Mauritania, kuwa njia sahihi ni kujaribu kusaidia masikini kwa misaada ya fedha, malengo maalum ya mpango wa kazi ili kupata chakula, na kuepuka ruzuku za jumla ambazo zinafuja mali na hazisaidii masikini.
►◄