1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa EU kujadili mzozo wa wahamiaji

23 Septemba 2015

Wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels kuujadili mzozo wa wahamiaji, baada ya mawaziri wa mambo ya ndani kukubaliana kugawana wakimbizi 120,000 waliopo katika nchi mfano wa Italia na Ugiriki

https://p.dw.com/p/1Gaqr
Kundi la wakimbizi wanaojaribu kuingia Ulaya ya Magharibi
Kundi la wakimbizi wanaojaribu kuingia Ulaya ya MagharibiPicha: Getty Images/AFP/S. Mitrolidis

Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wamepata muafaka juu ya mpango wa kugawana wakimbizi, lakini katika hali isiyo ya kawaida, muafaka huo ulipitishwa kwa wingi wa kura, na sio kwa kauli moja. Mpango huo ulipingwa na nchi za Ulaya Mashariki ambazo ni Jamhuri ya Czech, Hungary, Romania na Slovakia, na Finland ilijizuia kupiga kura yake. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema muafaka huo ni hatua ya uwajibikaji.

Amesema, ''Tumepata matokeo, baraza la mawaziri wa mambo ya ndani limeamua wakimbizi 120,000 waliopo Italia na Ugiriki watagawanywa miongoni mwa nchi za Ulaya, na Ujerumani itawapokea wapatao 30,000. Tunayafanya haya kama hatua ya mshikamano na uwajibikaji, lakini pia tunazingatia maslahi ya nchi zetu''.

Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere
Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de MaizierePicha: picture-alliance/dpa/D. Aydemir

Hiari iliyosindikizwa na shinikizo

Waziri wa mambo ya nje wa Luxembourg ambayo inashikilia uenyekiti wa kupokezana katika Umoja wa Ulaya, Jean Asselborn amesema muafaka umepatikana kwa kushinikiza kwa sababu wanakabiliwa na hali ya dharura. ''Kama tusingepata makubaliano, Ulaya ingekabiliwa na mgawanyiko zaidi'', amesema Asselborn.

Kutokana na kupatikana makubaliano hayo, mkutano wa wakuu wa nchi unaofanyika leo mjini Brussels utajikita zaidi juu ya kuimarisha ulinzi katika mipaka ya Umoja wa Ulaya, na kutoa msaada zaidi kwa nchi zilizo jirani na Syria, Uturuki, Jordan na Lebanon, pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Manung'uniko Ulaya Mashariki

Nchi za Ulaya ya Mashariki zilizopinga mpango huo, zimesema muafaka uliopatikana haukuwa hatua ya busara. Kupitia mtandao wa Twitter, waziri wa mambo ya ndani ya Jamhuri ya Czech Milan Chovanec, amesema, ''Punde tutamkuta mfalme bila ya chochote". Naye waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico amenukuliwa na vyombo vya habari akisema yuko radhi kuvunja sheria za Umoja wa Ulaya, kuliko kukubali kile alichokiita ''udikteta huu''.

Mzozo wa wakimbizi umesababisha mgawanyiko kimaoni katika Umoja wa Ulaya
Mzozo wa wakimbizi umesababisha mgawanyiko kimaoni katika Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Wijngaert

Kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya leo, Rais Barack Obama wa Marekani amezitaka nchi za Ulaya kuchukua wahamiaji kulingana na uwezo wa kila nchi.

Kauli hiyo ya Obama, ambayo imetangazwa baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, imechukuliwa kama onyo kwa nchi ambazo zinaweza kukaidi makubaliano yaliyofikiwa.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazaneuve amesema ingawa makubaliano yamechukua muda muda mrefu kupatikana, yamedhihirisha kuwa pale Ujerumani na Ufaransa zinapoamua kuweka shinikizo la pamoja na washirika wengine, na hasa panapokuwa na mzozo wa kibinadamu ambamo watu wanakufa majiano uamuzi unafikiwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Hamidou Oummilkheir