1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa majeshi wa ECOWAS kuijadili Niger

Saleh Mwanamilongo
15 Agosti 2023

Vyanzo vya kijeshi vinasema wakuu wa majeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Magharibi (ECOWAS) watakutana mjini Accra, Ghana siku ya Alhamis na Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4VCmd
Kikao cha viongozi wa majeshi ya ECOWAS kilikuwa kimepangwa kufanyika Jumamosi jijini Accra kabla ya kuhairishwa
Kikao cha viongozi wa majeshi ya ECOWAS kilikuwa kimepangwa kufanyika Jumamosi jijini Accra kabla ya kuhairishwa Picha: KOLA SULAIMON/AFP

Mkutano wa Alhamisi na Ijumaa wa wakuu wamajeshi ulikuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita lakini ukaahirishwa. Mkutano huo umekuja wiki moja baada ya Marais wa jumuiya ya ECOWAS kuamua kupelekwa kikosi cha dharura kumrejesha madarakai Mohamed Bazoum, rais wa Niger, aliyepinduliwa na jeshi Julai 26.

Wakuu wa jumuiya ya Ecowas walikutana katika mji wa Abuja nchini Nigeria Alhamis iliyopita ambapo walisisitiza malengo ya Jumuiya hiyo kutumia njia za kidiplomasia kuhusu kinachoendelea Niger. Huku wakitishia kutumia nguvu ya kijeshi.

Putin aomba suluhisho la amani

Wakati wa mazungumzo ya simu leo hii, Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Mali Assimi Goïta, ambaye aliingia madarakani kwa mapiduzi ya kijeshi mnamo 2020, walisisitiza umuhimu wa kutatua mzozo wa Niger, kwa njia ya amani, ya kisiasa na kidiplomasia. Mali, ambayo ni nchi jirani ya Niger, ilionyesha mshikamano wake na wanajeshi walioshika madaraka huko Niamey mara tu baada ya mapinduzi ya July 26.

Kufuatia uwezekano wa jumuiya ya ECOWAS kupeleka wanajeshi wake nchini Niger, viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo walitangaza kwamba watavishambulia vikosi vya nje endapo vitaivamia Niger na kutangaza kumfungulia mashtaka ya uhaini mkubwa rais Mohamed Bazoum.

''Tamko la kutia wasiwasi sana''

Viongozi wa kijeshi nchini Niger, wamewaita nyumbani mabalozi wake katika nchi za Ivory Coast na Nigeria
Viongozi wa kijeshi nchini Niger, wamewaita nyumbani mabalozi wake katika nchi za Ivory Coast na NigeriaPicha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Umoja wa Mataifa amesema mpango wa viongozi wa kijeshi wa Niger kumshitaki rais ni wa kutisha sana.

"Ni wazi kuwa ni tamko la kutia wasiwasi sana. Tunasalia na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya maisha, afya na usalama wa rais na familia yake, na tena, tunatoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja na bila masharti na bila shaka kurejeshwa kama mkuu wa nchi.",alisema Dujarric.

Tishio hilo la kisheria pia lililaaniwa vikali na jumuiya ya ECOWAS. Marekani ilisema imefadhaishwa sana na tangazo hilo la wanajeshi wa Niger. Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze, aliyeko ziarani katika eneo hilo la Afrika Magharibi, amekosoa hatua hiyo na kuelezea wasiwasi wa Ujerumani kuhusu usalama wa rais Bazoum na familia yake.

Katika tukio la hivi karibuni, uongozi wa kijeshi umemrejesha nyumbani balozi wa Niger mjini Abidjan kwa ajili ya mashauriano, baada ya matamshi ya Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara kusema yuko tayari kutuma wajaneshi wa nchi yake huko Niger.

Kiongozi huyo alisema Ivory Coast itachangia kati ya wanajeshi 850 na 1,100, pamoja na mataifa ya Nigeria na Benin.