Wakurdi wawaondoa Waarabu kwa nguvu Syria - AI
14 Oktoba 2015Mamalaka za serikali za mitaa zinazoongozwa na chama cha Kikurdi cha PYD nchini Syria, wana ushirikiano na Marekani katika vita dhidi ya vuguvugu la kijigadi la Waislamu wenye misimamo mikali.
Hata hivyo, Amnesty International inasema chama hicho kimekua kikitumia vibaya mamlaka yake pamoja na kukiuka sheria za kimataifa za kulinda ubinaadamu.
Wachunguzi wa shirika hilo walitembelea miji 14 pamoja na vijiji kadhaa kaskazini mwa Syria baina ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu na baadae kuandika ripoti kutokana na uchunguzi walioukusanya.
Na kwa mujibu wa Lama Fakih, mshauri muandamizi wa masuala ya migogoro wa shirika hilo, ripoti hiyo imekusanya ushahidi ulio wazi unaonesha utesaji wa makusudi wa raia katika vijiji ambayo awali vilishikiliwa na kundi la IS, au katika maeneo yanayotiliwa shaka ni makaazi ya wanaoliunga mkono kundi hilo.
Wakurdi wakana shutuma za Amnesty International
Zaidi shirika la Amnesty International limesema chama hicho kilijitetea kwa kusema raia hao walihamishwa kwa usalama wao wenyewe.
"Katika vita siku zote raia wanaumia, hilo linajulikana. Lakini suluhisho ni kuwaondoa mpaka mapigano yatulie, au mpaka wanamgambo wa IS waondolewe katika eneo hilo. Kufanya hivyo haina maana kuwa kulifanyika unyanyasaji ama kampeni ya kuwaondoa kwa nguvu raia katika makaazi yao," amesema Msemaji mkuu wa chama cha YPD,Redur Khalil.
Halikadhalika afisa mmoja wa Kikurdi aliyekataa kutajwa kwa jina, amesema kuwa sheria ndogondogo zilikiukwa dhidi ya watu waliotiliwa shaka wana mafungamano na IS, lakini visa hivyo havikuwa vya kikabila.
Aidha ripoti hiyo imethibitisha kuwa, jeshi la chama cha YPG, liliteketeza karibu nyumba zote katika kijiji kimoja ambacho kiliwahi kuwa chini ya udhibiti wa kundi la IS, kupitia ushahidi wa picha za satelaiti zinazoonesha hali ya kijiji hicho kabla na baada ya kuteketezwa.
Mafanikio ya Wakurdi dhidi ya IS
Wanamgambo wa kabila la Kikurdi nchini Syria, wamefanikiwa kudhibiti maeneo kadhaa kaskazini mwa nchi hiyo tangu kulipoanza vita mwaka 2011.
Kundi hilo la kikabila pia ni moja wapo ya makundi yaliyofanikiwa kupambana na vikosi vya kundi la IS. Kwa msaada wa mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani, wakurdi waliweza kulishinda kundi la IS katika mji wa Kobani ulioko karibu na mpaka wa Syria mapema mwaka huu. Lakini Lama Fakih anasema, wapiganaji hao Wakikurdi hawapigani tu na kundi la IS bali pia wanatesa raia wasio na hatia.
Mwandishi:Yusra Buwayhid
Mhariri:Josephat Charo