Wakurdi wapata mafanikio dhidi ya "Dola la Kiislamu"
15 Machi 2015Kwa mujibu wa taarifa ya afisa mmoja wa kikurdi na asasi ya wanaharakati, katika mapambano dhidi ya kundi linaloitwa Dola la Kiislamu, wapiganaji wa kikurdi wanaoshirikiana na wanamgambo wa Kikristo, wanapata mafanikio.
Afisa huyo Nasser Haj Mansour kutoka wizara ya ulinzi katika jimbo la wakurdi la nchini Syria, amesema wapiganaji wa kikurdi wamekiteka kijiji kimoja katika jimbo la Hassakeh ambacho hapo awali kilikuwa kinadhibitiwa na wapiganaji wa Dola la Kiislamu.
Afisa huyo pamoja na wawakilishi wa asasi inayofuatilia haki za binadamu nchini Syria kutokea London, wamesema wapiganaji wa Peshmerga walikiteka kijiji hicho usiku wa juzi.
Mapigano makali
Kwa mujibu wa taarifa ya pande hizo mbili, mashambulio ya ndege ya nchi zinazoongozwa na Marekani katika mfungamano dhidi ya Dola la Kiislamu,yaliwalenga wapiganaji wa Waislamu hao wenye itikadi kali kaskazini mashariki mwa Syria. Lakini pana taarifa ya mapigano makali.
Na Marekani imeeleza katika taarifa kwamba shambulio la ndege dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu karibu na mji wa Hassakeh lilikilenga kikosi cha mikakati cha Dola la Kiislamu na kukivuruga kabisa.
Kikosi muhimu cha wakurdi nchini Syria, Ijumaa iliyopita kiliiomba Marekani ifanye mashambulio ya ndege katika jimbo la Hassakeh. Wapiganaji wa waislamu wenye itikadi kali, wa Dola la Kiislamu,kwa muda wa wiki kadhaa, wamekuwa wanapambana na Wakurdi na wanamgambo wa Kikristo wa Syria katika jimbo la Hassakeh. Wapiganaji kadhaa walikufa katika kila upande.
Mashambulio ya ndege yawapa nguvu wakurdi
Katika miezi ya iliyopita mashambulio ya ndege ya nchi za mfungamano unaoongozwa na Marekani yaliwawezesha wapiganaji wa Kikurdi kuwatimua wanaoitwa wanajihadi wa Dola la Kiislamu katika mji wa Kobani, na tokea wakati huo wapiganaji wa Kikurdi wanaudhibiti mji wa Kobani kikamilifu. Majeshi wa Wakurdi pia yanavidhibiti vijiji kadhaa vinavyouzunguka mji huo.
Jeshi la wakurdi limetoa mwito kwa vijana wajiunge katika kupambana na Dola la Kiislamu kwa sababu jeshi hilo limeeleza kuwa waislamu hao wenye itikadi kali wameziongeza nguvu zao kwa kuwaingiza wapiganaji zaidi kutoka Syria na Iraq.
Wakati huo huo katika tamko la kukumbusha mwaka wa tano tokea kuanza vita vya nchini Syria mjumbe maalumu wa heshima wa Umoja wa Mataifa Angelina Jolie amezitaka serikali duniani kote ziweke kando tofauti zao ili ziutatue mgogoro wa nchini Syria kwa njia ya mazungumzo. Vita vya nchini Syria vimeshasababisha vifo vya watu zaidi ya 220,000.
Mwandishi:Mtullya Abdu.ape,
Mhariri:Gakuba Daniel