1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi wakubali jeshi la Syria kuingia mkoa wa Afrin

Sylvia Mwehozi
19 Februari 2018

Vikosi vya jeshi la kikurdi la Syria na vile vya serikali ya Damascus vimekubaliana kwa jeshi la Syria kuingia katika mkoa wa Afrin ili kuwasaidia kupambana na mashambulizi ya Uturuki.

https://p.dw.com/p/2suQN
Syrien Rakka Provinz Checkpoint Syrische Armee
Picha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Mshauri wa utawala unaongozwa na wakurdi katika eneo la kaskazini mwa Syria Badran Jia Kurd, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba vikosi vya jeshi vitasambazwa katika maeneo ya mpakani na vinaweza kuingia katika mkoa huo ndani ya siku mbili zijazo.

Mpango huo unapigia msumari vita inayozidi kuongezeka kaskazini mwa Syria, inayotokana na mtandao wa ushindani na ushirikiano miongoni mwa majeshi ya Kikurdi, serikali ya Syria, makundi ya waasi yaliyogawika, Uturuki, Marekani na Urusi.  Uhusiano mgumu baina ya serikali ya Damscus na vikosi vya jeshi la Kikurdi la Syria, ambayo kila mmoja anashikilia eneo zaidi dhidi ya upande mwingine katika vita, utakuwa na umuhimu namna mgogoro huo utakavyotatuliwa.

Syrien Afrin FSA Kämpfer
Mpiganaji wa jeshi huru la Syria katika mkoa wa AfrinPicha: Reuters/K. Ashawi

Ankara ilianzisha mashambulizi ya ardhini na angani katika mkoa wa Afrin mwezi uliopita ikawalenga wanamgambo wa wa kikurdi wa YPG, ambao inawachukulia kama kundi la kigaidi lenye mafungamano na kundi la waasi nchini Uturuki.

Marekani mshirika wa Uturuki katika jumuiya ya kujihami ya NATO imelipatia silaha kundi la YPG na kulifanya sehemu ya muungano wake inaouunga mkono nchini Syria dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu IS. Lakini wakati ambapo Marekani ina majeshi yake katika maeneo mengi nchini Syria ambayo yanadhibitiwa na kundi la YPG na washirika wake upande wa mashariki, Marekani haijaliunga mkono kundi hilo katika mkoa wa Afrin.

Ingawa serikali ya rais Bashar al-Assad na kundi la YPG wamekuwa wakiepuka mgogoro wa moja kwa moja, mara kadhaa wamepambana na wana misimamo tofauti kuhusu mustakabali wa baadaye wa Syria. Wakati pande zote zikipendekeza makubaliano ya muda mrefu kuwa jambo linalowezekana, rais Assad anasema anataka kuidhibiti tena nchi zima.

Syrien Afrin - Konflikt Türkei-Kurden
Moshi unaonekana kwa mbali katika mji wa Afrin SyriaPicha: Getty Images/AFP/A. Shafie Bilal

Hayo yakijiri, Uturuki imesema kwamba haijawahi kutumia silaha zenye kemikali katika operesheni zake nchini Syria na inachukua tahadhari kubwa kuwajali raia, amesema waziri wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu akiyaita madai yaliyotolewa na vikosi vya wakurdi na makundi ya uangalizi kuwa "yasiyo na msingi" kwamba Uturuki ilifanya shambulio la gesi katika mkoa wa Afrin. Akiwa katika mkutano wa usalama mjini Munich, Cavusoglu alisema nchi yake itaendeleza mapambano dhidi ya kundi la YPG, akigusia pia ushirikiano na Marekani. "Tutaanza na Manbij. Baada ya YPG kuondoka hapa tunaweza kushirikiana na Marekani kutokana na uaminifu. Lakini kwanza YPG inahitaji kuondoka mara moja. Hii ni ahadi tuliyopewa na Marekani na tutazungumza namna gani ahadi hii itakavyotimizwa wakati wa majaribio ya kuanzishwa kwa taratibu baina ya nchi hizi mbili," alisema Mevlut.

Serikali ya Syria imewaruhusu baadhi ya wapiganaji wa Kikurdi, raia na wanasiasa kuingia Afrin kupitia eneo lake, wawakilishi wa pande zote walililiambia shirika la habari la reuters katika wiki za karibuni.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters

Mhariri: Josephat Charo