Wakongo watumia mechi ya mpira kumkataa Kabila
16 Septemba 2016Gazeti la die tageszeitung, ambalo linasimulia kampeni ya wananchi wanaopingana na kile wanachosema ni azma ya Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kutaka kujiongezea muda wa kusalia madarakani, hata baada ya muhula wake kumalizika baadaye mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya sasa.
Gazeti hilo linasimulia mkasa mmoja, ambapo wananchi hao waliligeuza jukwaa la michezo kuwa sehemu ya kupaza sauti zao, wakati wa mechi kati ya timu ya taifa ya Kongo na ile ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, mwanzoni mwa mwezi huu.
Siku hiyo ya tarehe 4 Septemba, mashabiki 80,000 walijazana kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Kinshasa kuangalia mechi hiyo, lakini ghafla na kwa sauti moja wakasikika wakipiga mayowe: "Kabila yebela mandate na yo esili!" ikimaanisha: "Sikiliza Kabila, muda wako umekwisha!"
Hakika, linasema gazeti hilo, huu ulikuwa ni ujumbe mzito sana kutoka kwenye jukwaa la michezo. Itakumbukwa kuwa mdahalo wa kitaifa ambao uliokuwa ukiendelea nchini Kongo kati ya chama tawala na baadhi ya makundi ya upinzani umefikia makubaliano ya kuweko na daftari jipya la wapiga kura na uchaguzi wa rais uitishwe baada ya kukamilika uandikishaji wapigakura, hiyo ikimaanisha kwamba uchaguzi wa rais uliostahiki kuitishwa Novemba mwaka huu, unaweza kuahirishwa kwa miezi mingine kadhaa ijayo, kama si miaka.
Saratani ugonjwa wa kale
Berliner Zeitung, gazeti linalochapishwa katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, limechapisha wiki makala yenye kichwa cha habari: "Saratani si ugonjwa wa kisasa" likiakisi ile dhana potofu iliyokuwepo kuwa ugonjwa huo umezuka katika siku za karibuni duniani, kutokana na aina ya vyakula na mfumo wa maisha ya kisasa.
Gazeti linaandika kuwa matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Witwatersrand ya Johannesburg, Afrika Kusini, yamethibitisha kwamba ugonjwa wa saratani ulikuwapo miaka takribani milioni mbili iliyopita. Mafupa ya wanaadamu walioishi zama hizo imepimwa na watafiti wa taasisi hiyo na kugunduliwa kuwa waliuguwa kensa ya mifupa.
Mabaki ya mvulana wa miaka 13 aliyeishi karibu na mji huo wa kibiashara wa Afrika Kusini, miaka milioni na laki 9 na thamanini elfu iliyopita, katika jamii ya kibinaadamu iliyopewa jina la kisayansi la Australopithecus Sediba, inaonesha kuwa mtoto huyo aliuguwa na kufa kwa saratani.
Ugunduzi huu sasa unauwa ile dhana iliyokuwa ikikubalika kuwa maradhi ya saratani yalianza baada ya mapinduzi ya viwanda na ukuwaji wa sayansi na teknolojia katika eneo la vyakula na virutubisho.
Ukuwaji wa watu Afrika watisha
Gazeti la Frankfurter Allgemeiner lina makala refu sana juu ya kile linachokiita "Mjengeko wa umri barani Afrika". Linaandika kuwa endapo utabiri juu ya mustakabali wa ukuwaji wa idadi ya watu utafuatwa kama ulivyo, hapana shaka bara la Afrika litabakia kwenye macho yetu kila siku.
Limekuwa sio tena jambo lisilo la kawaida kusikia misamiati kama vile "bomu linalosubiri kupasuka" au "mripuko wa idadi ya watu", pale Afrika inapotajwa. Kufikia mwaka 2100, bara hilo litakuwa na mara nne ya idadi ya watu bilioni moja waliopo sasa.
Lakini je, hilo ni janga kwa maana zote? Anauliza mwandishi wa makala hii. Na jawabu lake ni kuwa wachumi na waandishi wa habari wanaoandikia "ukuwaji wa uchumi wa Afrika", wanajumuisha pia ukweli kuwa Afrika inaongeza idadi ya wakaazi wake. Kila watu wakiwa wengi, maana yake mahitaji yanakuwa mengi - walaji na watumiaji wanaongezeka.
Hata hivyo, wasomi wengi huhusisha ukuwaji huo na maharibiko ya kimazingira, kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Wazo likiwa moja: jeshi kubwa la wasio ajira miongoni mwa vijana wa Afrika litakuwa balaa kwa mataifa tajiri ya kizio cha kaskazini cha dunia.
Tumalizie uchambuzi huu wa magazeti ya Ujerumani wiki hii, kwa kufunua kurasa za gazeti la Süddeutsche Zeitung kwenye safu yake ya uhakiki wa vitabu, ambapo safari hii kinahakikiwa kitabu "Tram 83" yaani Treni Namba 83 cha Fiston Nasser Mwanza Mujila, mwandishi wa riwaya wa Kongo, ambaye anaishi sasa nchini Austria.
Taswira ya kituo cha treni cha City State barani Afrika, anasema mhakiki wa Süddeutsche Zeitung, ni kielelezo cha uhalisia wanaoishi nao watu kila siku. Kituo chenyewe ni kama karakana, ghala la vyuma chakavu, vichwa vichache vya matreni makuukuu, na kwa ujumla ghasia, fujo na ujuwaji.
Mhakiki ananukuu kauli ya abiria mmoja akimwambia mgeni: "Hapa kituoni na humo ndani ya Treni Namba 83, ni porini. Kama hukutenda, utatendwa, kama hukula, utaliwa. Usipovuta pumzi, utamalizwa.."
Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Süddeutsche Zeitung, Frankfurter Allgemeiner, Berliner Zeitung/die Tageszeitung
Mhariri: Saumu Yussuf