Wakimbizi wapewa hifadhi Ujerumani
4 Mei 2015Wakimbizi 480 watapelekwa katika kitongoji cha Berlin -Buch ngwazoni kidogo mwa jiji la Berlin. Wakimbizi hao wanatoka Kosovo, Palestina,Eritrea na Syria.
Eias Bieasssy kutoka Syria ni miongoni mwa wakimbizi hao na amefurahi sana kupewa hifadhi nchini Ujerumani. Mkimbizi huyo mwenye umri wa miaka 37 alipitia Misri,Italia na Uturuki ili kufika Ujerumani.
Amesema njia hiyo ni ndefu lakini ni ya usalama zaidi .Licha ya hayo aliamua kuwaacha nchini Syria mke na mtoto wake mchanga. Bieassy alipata habari juu ya maafa yaliyowafika wakimbizi zaidi ya 800 kwenye bahari ya Mediterania. Lakini amefurahi kufika Ulaya na amesema kuwa Ujerumani ni nchi nzuri.
Kwa nini wakimbizi wapelekwe katika mji wao?
Hatahivyo baadhi ya Wajerumani katika mji ambako wakimbizi wamepewa hifadhi wanauliza kwa nini wakimbizi hao wapelekwe katika mji wao.?
Kitongoji cha Berlin - Buch kilichopo mashariki mwa jiji la Berlin hakiwezi kuhesabika kuwa mahala pa mchanganyiko wa tamaduni. Nyumba ya wakimbizi imejengewa kuta mbili siyo kwa ajili ya kuwafungia wakimbizi ndani bali kwa ajili ya usalama wao. Kitongoji cha Berlin - Buch hakina mazoea na wakimbizi na wapo Wajerumani wenye siasa kali wanaowachukia wageni.
Waziri azitaja sababu za ukimbizi
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maizere amezitaja sababu zinazowafanya watu wazikimbie nchi zao. Amesema umasikini,maonevu na uhalifu ndizo sababu zinazowafanya watu wazikimbie nchi zao. Na kwa hivyo ameeleza kwamba panahitajika jibu linaloyazingatia mambo hayo matatu.
Kambi ya wakimbizi katika sehemu ya Berlin -Buch imeshawahi kushambuliwa na watu wenye siasa kali. Wakimbizi 75 wa kwanza waliowasili katika sehemu hiyo walisongwasongwa na kutupiwa chupa. Sasa polisi wamewekwa mbele ya nyumba ya wakimbizi hao. Watu wenye siasa kali walitaka kufanya maandamano mengine ya kuwapinga wakimbizi hao.
Wakimbizi hao wanaishi katika makontena. Hata hivyo jambo la kutia moyo ni kwamba wapo wakaazi wa kitongoji cha Berlin-Buch wanaowasaidia wakimbizi hao. Eias Bieasssy ameweza kujionea mwenyewe ukarimu na urafiki wa Wajerumani hao. Wajerumani hao waliandaa tafrija kwa ajili ya kuwakaribisha wageni hao kutoka nchi mbalimbali.
Wakaazi wa mji wa Berlin-Buch zaidi ya150 wanawasaidia wakimbizi hao kwa namna mbalimbali. Wanawafunza lugha ya kijerumani,wanawasaidia kuwalea watoto na mara nyingine wanatembea pamoja nao ili kuwaonyesha mji.
Mwandishi:Kiesel ,Heiner
Mfasiri:Mtullya Abdu.
Mhariri: Yusuf Saumu