1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Somalia walazimishwa kurejea makwao

31 Machi 2012

Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za binaadamu - Human Rights Watch limesema serikali ya Kenya haipaswi kuwarejesha wakimbizi nchini Somalia kwa sababu bado kuna mapigano yanayoendelea nchini humo.

https://p.dw.com/p/14V7o
Children lay on beds at Banadir hospital in Mogadishu, Somalia, Monday, Aug 1, 2011.Tens of thousands of famine-stricken Somali refugees were cold and drenched after torrential rains overnight pounded their makeshift structures in the capital, Mogadishu. Rains are needed to plant crops and alleviate the drought that is causing famine in Somalia but on Saturday night the rains added to the misery of refugees who live in structures made of sticks and pieces of cloth. (A Photo/Farah Abdi Warsameh)
Somalia Hungersnot Lager Flüchtlingslager KinderPicha: dapd

Shirika hilo limesema badala ya Kenya kudai kuwa "maeneo hayo yaliyokombolewa upya" ni salama kwa wakimbizi kurejea, inafaa kufungua upya kituo cha ukaguzi huko Liboi na kuendelea kuwasajili wakimbizi wapya ili kuhakikisha wanapatiwa msaada.

Katika miezi kadhaa iliyopita, maafisa maarufu nchini Kenya wamewataka wakimbizi wa Kisomali kurejea nchini mwao, wakidai kuwa ni salama kwao kurudi. Katika wiki ya tarehe 19 mwezi Machi mwaka huu Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wakati huo Moses Wetangula na Waziri wa Usalama wa Ndani George Saitoti walisema kuwa jeshi la Kenya limeunda neo ndani ya Somalia ambalo ni salama kwa wakimbizi waanorejea, wakisisitiza matamshi ya Rais Mwai Kibaki katika kongamano la London kuhusu Somalia mnamo Februari 23.

Vita dhidi ya al-Shabaab vyaendelea

Hata hivyo hilo limesema mapigano bado yanaendelea katika miji ya mipaka na sehemu ambazo Kenya inadai kuzidhibiti, na kundi la wanamgambo la Kiislamu al-Shabaab liko katika maeneo hayo.

Vikosi vya Kenya vinavyopambana na al-Shabaab Somalia vilijumuishwa katika kundi la AMISOM
Vikosi vya Kenya vinavyopambana na al-Shabaab Somalia vilijumuishwa katika kundi la AMISOMPicha: AP

Wakati serikali ikisema kurejea kwa wakimbizi hao ni wka hiari, shirika la Human Rights Watch linasema liliwahoji baadhi ya waathiriwa walionyanyaswa na polisi katika kambi ya Daadab mwezi Desemba mwaka uliopita, ambapo watatu ya wale waliopigwa waliambiwa na polisi warejee kwao Somalia. Shirika hilo linasema kuwalazimisha wakimbizi kurejea katika nchi ambayo wanakabiliwa na mateso, na ghasia za jumla kama vile Somalia, kunakiuka sheria ya kanda ya Afrika na Kimataifa.

Utafiti wa Human Rights Watch hata hivyo ulibaini kuwa kumekuwa na mapigano ya kila mara baina ya vikosi vya pamoja vya Kenya na washirika wake Somalia na wanamgambo wa al-Shabaab katika jimbo la Juba chini linalodhibitiwa na wanajeshi wa Kenya. Wakaazi wawili wa Bills Qogaani , kilomita 90 kutoka mji wa Dhobley ulio katika mpaka wa Kenya na Somalia waliliambia shirika hilo kuwa wapiganaji wa al-Shaabab waliushambulia mji huo mnamo Machi 17. Mkimbizi kutoka kijiji cha Somalia cha Taabta kilomita 60 kutoka Dhobley naye alisema alilazimika kutoroka mnamo machi 15 kutokana na mashambulizi ya usiku ya al-Shaabab katika kambi iliyo karibu ya jeshi la Kenya.

Maelfu ya raia wametoroka makwao

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa maelfu ya raia wa maeneo ya Gedo na Juba ya chini wamepoteza makaazi yao ikiwemo miji inayodaiwa kuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Kenya na vile vya serikali ya mpito ya Somalia.

Wakimbizi wengi wa Kisomali inazidi kumiminika katika kambi za wakimbizi Kenya
Wakimbizi wengi wa Kisomali inazidi kumiminika katika kambi za wakimbizi KenyaPicha: picture alliance/dpa

Chanzo kimoja cha habari kililiambia human rights watch kuwa vikosi hivyo vimedhibiti shule katika eneo la Gedo na kufanya kuwa vigumu masomo kuendelea.

Shirika hilo linasema wakati serikali ya Kenya ina sababu za msingi kuhusu athari ya kimazingira na kiusalama katika kuwapa hifadhi mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa Somalia, sababu hizo haziwezi kuhalalisha kuwahimiza wakimbizi kurejea katika eneo la vita.

Shirika hilo limesema Kenya inafaa kuimarisha usalama wa wakimbizi na jamii katika eneo la Daadab kwa kuchunguza na kuwashitaki maafisa waliofanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu hivi karibuni dhidi ya wakimbizi, ukiwemo uvamizi wa polisi mwezi Desemba ambapo zaidi ya wakimbizi 100 walipigwa.

Mwandishi: Bruce Amani/HRW

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman