1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa somalia wakataa kurejea kwao

13 Oktoba 2016

Zaidi ya wakimbizi wanane wa Somalia kati ya kumi wanaoishi kwenye kambi ya Dadaab, hawataki kurejea nchini mwao, kutokana na kitisho cha kubakwa, kulazimishwa kupewa mafunzo ya uanamgambo na ukosefu wa huduma za afya

https://p.dw.com/p/2RCKM
Kenia Das Flüchtlingslager Dadaab
Picha: picture alliance/dpa/UNHCR/B. Bannon

Shirika la madaktari wasio na mipaka, Medecins Sans Frontieres, MSF limesema kurejeshwa kwa wakimbizi 300,000 raia wa Somalia, nchini humo waliokuwa wakiishi kwenye kambi ya Dadaab kunaweza kuwa ni janga kubwa kwa afya zao, kwa kuwa kunawaweka kwenye hatari ya kupata maradhi yatokanayo na utapiamlo na magonjwa ya kuambukiza kama Polio.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, Kenya inahudumu kambi hiyo kubwa zaidi duniani, ikiwa na wakimbizi wengi kutoka nchini Somalia, waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 25. Kenya na Umoja wa Mataifa, kwa pamoja wamesema urejeshwaji huo unazingatia zaidi hiyari ya wakimbizi, ambapo huchukuliwa na kupelekwa kwenye maeneo salama yaliyoandaliwa.

Wameomba misaada zaidi kutoka kwa wahisani ili kuwezesha utoaji wa huduma bora zaidi za afya na elimu nchini Somalia. Kenya imesema haina budi kuifunga kambi hiyo ya Dadaab kwa kutilia maanani suala la usalama nchini mwake, kutokana na kambi hiyo kutumiwa na magaidi kama mwanya wa kuingia na kufanya mashambulizi ya kutisha nchini Kenya.

Watoto wanaoingia nchini Kenya wakitokea Somalia, hawajawahi kupata chanjo za kawaida za watoto, shirika hilo la MSF limesema. Na wengi wa watoto wanaofika nchini humo hupatikanika wakiugua maradhi ya surua 

Symbolbild Frauen Vergewaltigung Not Hunger Armut in Somalia
Baadhi ya wakimbizi wa Somalia wakiwa kwenye eneo la kuandikishwa kupata kibali cha kuishi kwenye kambi ya Dadaab.Picha: Oli Scarff/Getty Images

Ugonjwa wa Polio ambao tayari ulikuwa umekwishatokomezwa kwa kiasi kikubwa duniani kupitia chanjo, iliripuka kwa mara nyingine mnamo mwaka 2014 nchini Somalia, hali iliyoashiria uwepo wa huduma duni ya afya nchini humo.

Nchini Somalia huduma za kliniki binafsi hutolewa kwa gharama ya juu mno na maduka ya dawa huwa yakiishiwa, na hata zile zinazouzwa huwa ni za kiwango cha chini, wakimbizi takriban 800 wanaoishi Dadaab wameliambia shirika hilo la MSF, walipofanyiwa mahojiano mnamo mwezi Julai na Agosti. Kwenye maeneo yasiyofikika kwa urahisi nchini humo, watu hulazimika kutegemea zaidi dawa na tiba za miti shamba, walisema.

Wakimbizi watatu kati ya kumi ya waliofanyiwa mahojiano na MSF wana mwanafamilia anayehitaji huduma ya afya kwa maradhi sugu kama pumu, kisukari na shinikizo la damu. Hufanikiwa kupata huduma za chini , MSF imesema. Na kwa wagonjwa wa kifua kikuu ambao tiba yao hukatishwa huwa kwenye hatari ya kutengeneza usugu wa dawa. 

Wawili kati ya wakimbizi kumi waliohojiwa wana mwanafamilia aliyehitaji huduma ya afya ya akili, ambayo upatikanaji wake pia ni duni nchini humo. MSF imetoa mwito kwa Kenya, wahisani na Umoja wa Mataifa kuangazia namna nyingine ya kupata suluhu, ikiwa ni pamoja na kuwatafutia hifadhi nchi nyingine, kuwahusisha na jamii nyingine nchini Kenya na ujenzi wa makambi madogo yanayoweza kutunzwa kiurahisi.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE.
Mhariri: Saumu Yusuf