Wakimbizi wa ndani waongezeka mara tatu Afrika
26 Novemba 2024Waangalizi wa kimataifa wamesema kwamba mizozo, machafuko na majanga kote barani Afrika yameiongeza mara tatu idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao barani humo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika linalofuatilia mienendo ya watu kulazimika kuyahama makazi yao ndani ya nchi zao, IDMC, kufikia mwisho wa mwaka uliopita, bara la Afrika lilikuwa na watu milioni 35 wanaoishi nje ya makazi yao katika nchi zao.
Mkuu wa shirika hilo Alexandra Bilak amesema idadi hiyo ni karibu nusu ya idadi jumla ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao ulimwenguni kote.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa mafuriko yalisababisha zaidi ya asilimia 75 ya ukimbijia na uhamaji huu, huku ukame ukiwasukuma wengine asilimia 11 kuyahama makazi yao.