1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi kupewa haki zaidi Ujerumani

Elizabeth Shoo6 Novemba 2014

Bunge la Ujerumani linajadili kuhusu sera za watu wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi hapa nchini. Pamoja na hayo, wabunge pia wanazizungumzia sheria za wakimbizi zilizowekwa na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1DiFm
Wakimbizi waliovuka bahari kwa boti
Picha: picture-alliance/ROPI

Wizara ya uhamiaji na wakimbizi hapa Ujerumani inakadiria kwamba katika miaka ijayo, zaidi ya watu 200,000 kwa mwaka wataomba hifadhi ya ukimbizi hapa Ujerumani. Hiyo inamaanisha kuwa idadi ya wakimbizi katika miaka ijayo itakuwa mara mbili ya idadi ya wakimbizi waliokuja Ujerumani mwaka uliopita. Wakimbizi 435,000 walisajiliwa katika nchi zote za Umoja wa Ulaya mwaka uliopita. Asilimia 70 ya wakimbizi hao walipokelewa na Ujerumani, Italia, Uingereza, Sweden na Ufaransa.

Sheria za Umoja wa Ulaya zinasema kwamba wakimbizi lazima waombe hifadhi katika nchi ya kwanza ya Umoja wa Ulaya wanayofikia. Ni jambo linaloyatwika mzigo mkubwa mataifa ya kusini mwa Ulaya kama vile Italia. Wakimbizi nchini humo wamekuwa wengi mno. Hivyo Italia imeamua kuwapa baadhi ya wakimbizi ruhusa ya kuhamia nchi nyingine za Umoja wa Ulaya kwa sababu wengi wanaowasili Ulaya kwa boti wakivuka bahari ya Meditarranean wanafikia Italia kwanza.

Sheria ya kazi kulegezwa

Mjadala mkubwa umezuka ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu namna ya kuwatawanya wakimbizi miongoni mwa mataifa mwanachama. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maizère, amependekeza kwamba idadi ya wakimbizi wanaopokelewa na nchi fulani inatakiwa iwe katika uwiano na idadi ya wakazi wa nchi hiyo. Hivyo nchi kama Ujerumani itapaswa kupokea wakimbizi wengi kuliko taifa dogo kama Malta. Wanaopinga wazo hilo wanakumbusha kwamba zipo nchi nyingi zenye wakazi wengi ambazo ni maskini huku mataifa kama Luxemburg yenye wakazi wachache kabisa yaikiwa tajiri na hivyo na uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia wakimbizi.

Bunge la Ujerumani linatarajiwa kupitisha sheria za kurahisisha maisha ya wakimbizi
Bunge la Ujerumani linatarajiwa kupitisha sheria za kurahisisha maisha ya wakimbiziPicha: imago/IPON

Iwapo sheria ya hapa Ujerumani itabadilishwa, wakimbizi watakuwa na haki ya kupewa fedha za matumizi. Kwa sasa mikoa mingi inawapatia watu hao mahitaji ya kila siku kama vile nguo na chakula na pia inawapa kuponi zinazowaruhusu kupata huduma fulani kama vile kwenda hospitalini au kuhudhuria masomo ya lugha.

Sheria mpya ikipitishwa itawarahishia pia wakimbizi kufanya kazi hapa nchini. Kwa mujibu wa sheria hiyo, wataweza kuanza kazi miezi mitatu baada ya kuwasili hapa. Kwa sasa, wanatakiwa kusubiri miezi tisa. Lakini sheria ambayo haitabadilika ni kwamba mkimbizi haruhusiwi kuchukua nafasi ya Mjerumani au raia wa Umoja wa Ulaya. Hivyo kama imetangazwa nafasi ya kazi ya ualimu kwa mfano, lazima ichunguzwe kwanza kama kuna mtu ambaye si mkimbizi atakayeweza kuchukua nafasi hiyo.

Mwandishi: Heiner Kiesel

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf