1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi 500 watoroka machafuko DRC na kuingia Uganda

Lubega Emmanuel14 Februari 2019

Mapigano ya kikabila yaliyotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC wiki iliyopita, yamesababisha zaidi ya watu 500 kukimbilia usalama nchini Uganda.

https://p.dw.com/p/3DME0
Picha ya maktaba: Wakimbizi kutoka DRC waliovuka ziwa Albert kuingia Uganda Machi 19, 2018.
Picha ya maktaba: Wakimbizi kutoka DRC waliovuka ziwa Albert kuingia Uganda Machi 19, 2018.Picha: Reuters/J. Akena

Zaidi ya raia 500 wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamewasili Uganda wakikimbia mapigano ya kikabila yaliyozuka wiki iliyopita. Wakimbizi hao wamewafahamisha maafisa wa Uganda pamoja na Shirika la Umoja Mataifa linalowahudumia Wakimbizi, UNHCR kwamba mapigano hayo yaliyozuka kati ya jamii za Lendu na Bagerere yamelitumbukiza eneo la mashariki mwa Congo katika hali ya sintofahamu.

Makundi hayo ya wakimbizi kutoka jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia yanafanya safari za hatari kuvuka Ziwa Albert lililoko kwenye mpaka wa nchi hizo mbili wakitumia mitumbwi isiyokuwa imara. Wengi wao ambao ni wanawake na watoto wameshuhudiwa wakiwa na mizigo yao hususan magodoro.

Kwa mujibu wa wakimbizi hao, mapigano hayo ni kati ya kikabila kati ya jamii ya Lendu na Bagerere. Kinachowatia hofu na wasiwasi viongozi wa wilaya za Hoima na Kikuube zaidi ya ambako wakimbizi 500 tangu Jumapili usiku ni uwezekano wa kuzorota kwa hali ya usalama. Inahofiwa huenda kuna uwezekano wa wakimbizi kuingia Uganda wakiwa wamejihami kwa silaha.

Picha ya maktaba
Picha ya maktabaPicha: Getty Images/AFP/A. Huguet

Mashaka mengine ambayo wimbi hilo jipya la wakimbizi kutoka DRC ni kuhusiana na jinsi watu hao wanawasili bila kupitia njia rasmi za mipakani ambako wangepimwa kabla ya kutangamana na jamii za Uganda.Wakaazi wana wasiwasi kuwa kuna uwezekano wa miripuko ya magonjwa ya Ebola na kipindupindu, kwani wanatokea sehemu ambako miripuko hiyo imeripotiwa hivi karibuni mashariki mwa nchi yao.

Uganda imeitikia hali hiyo kwa kutuma majeshi kuhakikisha usalama maeneo ya mpakani hasa kwenye fukwe za Ziwa Albert huku makundi ya maafisa wa afya wakipelekwa kuwapima wakimbizi hao kabla ya kuwasafirisha kwenda kwenye kambi rasmi ya wakimbizi ya Kyangwali.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi limefafanua kuwa hata kabla ya kundi hilo la wakimbizi kuanza kuwasili Uganda, kila siku kiasi ya watu 113 wamekuwa wakiwasili kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Inakisiwa kuwa kuna wakimbizi 240,000 kutoka nchi hiyo jirani walioko Uganda, idadi kubwa ikiwa imetokea majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.

Mhariri: Grace Patricia Kabogo