Wakenya wapiga kura kumchagua rais mpya
8 Agosti 2017Rais Uhuru Kenyatta, mwana wa rais wa kwanza wa Kenya, anagombea muhula wa pili dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga, ambaye ni mwana wa Makamu wa rais wa kwanza wa nchi hiyo.
Baada ya miezi miwili ya kampeni zilizojaa maneno makali lakini hotuba za umma ambazo kwa kiasi kikubwa hazikugusia hisia za chuki za kikabila ambazo zilizigubika chaguzi za awali, uchunguzi wa maoni umewaweka wagombea hao katika kinyang'anyiro kikali.
Matokeo ya mwanzo hayatarajiwi kutolewa kabla ya kesho Jumatano, lakini kiyang'anyiro kikali huenda kikamaanisha kuwa mshindi ataibuka baada ya hata siku tatu. Kwa mujibu wa katiba, tume ya uchaguzi ina hadi siku saba kumtangaza mshindi.
Maelfu ya raia wamehama mijini kwenda mashambani kabla ya uchaguzi wakihofia kuzuka ghasia kama za mwaka wa 2007. Ngome za wafuasi wa Odinga anayewakilisha muungano wa upinzani - NASA ni magharibi mwa Kenya pamoja na pwani, wakati Kenyatta wa chama cha Jubilee ana ngome za wafuasi katika eneo la Kati na Bonde la Ufa.
Serikali imewaweka Zaidi ya maafisa wa usalama 150,000 wakiwemo askari wa wanyamapori, kuvilinda vituo 41,000 vya kupigia kura kote nchini. Tume ya uchaguzi – IEBC inasisitiza kuwa imefanya majaribio yote ya kulinda zoezi la kujumlisha na kutangaza matokeo.
Kuna Zaidi ya waangalizi 6,000 wa uchaguzi huo kutoka ndani na nje ya nchi na mawakala wa vyama katika kila kituo watahitajika kusaini matokeo ya kura ambayo kisha yatatumwa kwa njia ya elektroniki kwa ofisi za kaunti na kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura jijini Nairobi. Pamoja na rais mpya, Wakenya pia wanawachagua wabunge na wawakilishi wa serikali za mitaa.
Jamii ya kimataifa inafuatulia kwa makini uchaguzi huo huku wito wa Amani ukitolewa. Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alijiunga na rais wa wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki anayeongoza ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika, na waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, katika kutaka uchaguzi wa Amani na wa haki.
Rais Uhuru Kenyatta alitoa hotuba kwa njia ya televisheni katika mkesha wa uchaguzi na kupunguza hofu, baada ya kukamilika kampeni zilizojaa madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi, yaliyotolewa na mpinzani wake Raila Odinga, na mauaji ya afisa mwandamizi wa uchaguzi.
Kenyatta amewataka wapiga kura milioni 19 waliosajiliwa kujitokeza kwa wingi na kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia kwa njia ya Amani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Zainab Aziz