Wakenya walalamikia ongezeko la bei ya sukari
10 Novemba 2021Hayo yanajiri wakati serikali ikijitahidi kuvifufua viwanda vyake vya sukari.
Serikali kuu ya Kenya imesema iliipa kampuni ya sukari ya Nzoia shilingi milioni 500 ili kukifufua kiwanda hicho kinachochechemea.
Fedha hizo ni sehemu ya kiwango cha shilingi bilioni 1.5 zilizotengwa na Wizara ya fedha kuvipa uhai mpya viwanda vya sukari vya serikali vilivyoko eneo la magharibi vinavyopitia wakati mgumu.
Peter Munya ambaye ni Waziri wa Kilimo wa Kenya na aliwakabidhi viongozi wa kampuni ya sukari ya Nzoia hundi hiyo.
Madeni yazonga viwanda vya sukari Kenya
Kampuni ya sukari ya Nzoia ina madeni makubwa. Wakulima wanaidai shilingi milioni 743, wasafirishaji shilingi milioni 182.4 nao wavunaji miwa wanasubiri kulipwa shilingi milioni 71.3.
Kwa sasa gunia moja la sukari la kilo 50 linauzwa kwa shilingi 6,200 kutokea shilingi 5,050 iliyokuwa bei ya mwezi uliopita. Ongezeko hilo la bei linawatatiza wakaazi ambao tayari wanakabiliana na hali ngumu ya maisha.
Soma: Bei ya mafuta yapanda maradufu nchini Kenya
Kulingana na taarifa, hali hii imesababishwa na misukosuko kwenye viwanda vya sukari. Kadhalika uuzaji wa sukari ya magendo pia umechangia kuivuruga hali ya wakulima wa miwa wanaotapatapa.
Kaunti ya Busia ni moja ya maeneo muhimu ya kilimo cha miwa na biashara ya sukari.
Takwimu za idara rasmi ya takwimu nchini Kenya zinaashiria kuwa bei ya sukari imeongezeka kwa asilimi 2.5 kutokea shilingi 111 hadi 114 kwa kilo moja.
Changamoto za kiufundi zatatiza viwanda
Katika miezi ya Agosti na Septemba, baadhi ya viwanda vilitatizwa na vikwazo vya kiufundi baada ya mashine kuharibika au kufungwa ili kuupa nafasi ukarabati.
Soma: Sakata la sukari yenye zebaki Kenya
Mashine za viwanda vya Chemelil na Kibos ziliharibika jambo lililosababisha miwa kulimbika na kukipunguza kiwango cha sukari kwenye soko la jumla.
Kwa upande mwengine wakulima walisalia na zaidi ya tani 14,000 za miwa iliyoendelea kukauka mashambani.
Wakati huohuo foleni ndefu za matrekta zimeshuhudiwa kwenye vituo vya kupima miwa hali inayovuruga utengenezaji wa sukari na hatimaye kuzua uhaba sokoni.