Uhuru awaongoza Wakenya kumuaga hayati Daniel arap Moi
8 Februari 2020Shughuli hii itaendelea kwa siku tatu mfululuzo kwa wikendi hii hadi Jumatatu. Hayati Mzee Moi alivishwa suti maalumu ya samawati iliyokolea na kulazwa kwenye sehemu maalumu alikotengewa kwenye majengo ya bunge. Maafisa wa jeshi la Kenya, KDF, wanapiga doria ndani na nje ya sehemu hiyo kama ilivyo ada.
Jeneza la bendera
Jeneza la hayati Mzee Moi lililofunikwa kwa bendera ya taifa lilisafirishwa mapema hii leo kutokea hifadhi ya maiti ya Lee iliyoko jijini Nairobi. Msafara huo ulipitia barabara ya Valley hadi ya Kenyatta na hatimaye ile ya bungeni. Muda baada ya kuwasili aliandaliwa gwaride la heshima kwani alikuwa amiri jeshi mkuu.
Rais Uhuru Kenyatta na mkewe Margaret ndio walioiongoza shughuli ya kitaifa ya kutoa heshima za mwisho kwa hayati Mzee Moi bungeni. Naibu wa rais, William Ruto, baraza la mawaziri na viongozi wengine wa ngazi ya juu walipewa muda wa saa nzima kutoa heshima zao kabla ya umma kuruhusiwa kuingia ndani.
Uhuru amsifu Moi
Rais Uhuru alimmiminia sifa Hayati mzee Moi alipotoa hotuba yake hii leo. Alimsifu Mzee Moi huku akimtaja kuwa "mwana mashuhuri wa Kenya, ndugu aliyependwa, baba mwenye upendo, mshauri wa wengi, Baba wa Taifa na mtetezi wa Uafrika."
Rais Kenyatta alisema Rais huyo wa zamani alikuwa kiongozi mashuhuri aliyetekeleza jukumu kubwa katika kupigania uhuru wa Kenya na kutumia muda mwingi wa maisha yake kulihudumia taifa hili. "Jua limetua kwa mtu aliyekuwa wa ajabu. Kiongozi mwenye hekima na huruma. Mwanadiplomasia mwanana na imara. Mtu aliyelihudumia taifa kwa ungwana na heshima. Rais ambaye hekima na ujuzi wake mkuu wa diplomasia uliiwezesha Kenya kutoegemea upande wowote, nyakati ambapo ulimwengu mzima ulikuwa umejitosa katika mgawanyiko wa Vita Baridi," alisema rais.
Alimsifu Mzee Moi kuwa kiongozi imara ambaye nyakati harakati za vyama vingi, alizisikiliza pande zote na kuandaa jukwaa ili kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi. "Alikuwa kiongozi mwerevu, ambaye wakati wa tetesi za katiba mpya, alisikiza na kimya kimya akachagua kilichokuwa bora kwa nchi hii," alisema Rais Kenyatta.
Kiongozi wa Taifa alimtaja Rais huyo wa zamani kuwa kiongozi mwenye maono aliyeondoka mamlakani kwa amani pale chama chake kilipopoteza uchaguzi mwaka wa 2002. "Hadi siku yake ya mwisho mamlakani, alibaki kujitolea na tayari kulilinda bara la Afrika na watu wake. Aliamini, kwa dhati, kwamba tuna suluhisho kwa matatizo yaliyolikumba bara letu,” aliongeza kusema Rais.
Ulinzi mkali
Maafisa wa usalama wa vitengo vyote walionekana wakipiga doria na kuliwekea vizuizi eneo linaloelekea bungeni kutokea pande zote katikati ya jiji. Foleni ndefu zilishuhudiwa wakati ambapo Wakenya wa kawaida walisubiri zamu ya kutoa heshima zao za mwisho.
Zilikuweko foleni mbili za wanawake na wanaume. Kila mmoja alilazimika kuzima simu na kuivua saa ya mkononi kuuondoa uwezekano wa kupiga picha zozote kwenye eneo alikolazwa Hayati mzee Moi. Maafisa wa usalama walimkagua kila aliyetaka kuingia kwenye majengo ya bunge na hata mikoba kupekuliwa. Wengi ya waliofika hapo walikuwa wanaume.
Siku ya mapumziko
Ili kuwapa nafasi Wakenya kushiriki kwenye ibada maalum ya mazishi, serikali imetenga siku ya Jumanne tarehe 11 mwezi wa Februari kuwa ya mapumziko. Ibada hiyo itafanyika kwenye uwanja wa michezo wa Nyayo ulioko mkabala na barabara ya Uhuru jijini Nairobi. Hayati mzee Moi aliyefariki dunia mwanzoni mwa wiki hii akiwa na umri wa miaka 95 atazikwa kwake nyumbani eneo la Kabarak, kaunti ya Nakuru tarehe 12 mwezi wa Februari.