Wakati watu wote wakisubiri matokeo ya urais, Vyama viwili vya Upinzani vya ungana nchini Zimbabwe.
28 Aprili 2008Wakati huo huo Chama Kikuu cha Upinzani cha Movement for Democratic Change -MDC kwa mara nyingine tena kimeendelea kupinga kurudiwa kwa uchaguzi.
Wakati wananchi wa Zimbabwe wakisubiri kuona ikiwa Tume ya Uchaguzi itatangaza matokeo ya Urais chama Kikuu cha Upinzani cha Movement for Democratic Chagnge -MDC, kimeungana rasmi na chama pinzani kinacho ongozwa na Arthur Mutambara.
Viongozi hao wawili Morgan Tsvangirai na Arthur Mutambara, wamezungumza katika mkutano na waandishi wa habari nchini Afrika kusini na kutangaza kwamba chama chao sasa kinawingi wa vitti Bungeni baada ya kuchukua hatua ya kuungana.
Kwa hivi sasa hata hivyo macho yote yanaelekezwa kwenye matokeo ya urais nchini Zimbabwe baada ya Tume ya Uchuguzi ya nchi hiyo kuahidi kuwa ingetangaza leo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe ilitangaza kuwa leo ingeweza kutoa matokeo ya uchaguzi lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote ya urais yaliyokwisha kutolewa.
Gazeti moja linalomilikiwa na Serikali limesema wawakilishi wa rais Robert Mugabe na wale wa kiongozi wa Upinzani Morgan Tsvangirai watakaribishwa katika wakati wa kutolewa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi.
Hata hivyo kwa upande wake chama cha MDC, kimesema kuwa hakijapata mwaliko wala mawasilliano yoyote kutoka Tume ya Uchaguzi.
Maafisa wa Kamati ya Uchaguzi nchini Zimbabwe walisema hadi kufikia leo wangekuwa wamekamilisha uchaguzi katika majimbo yaliyokuwa yamesalia na hivyo kufanya wagombea wote kuanza kupitia matokeo.
Ni majuma manne sasa yamepita tangu uchaguzi kuu ufanyike nchini Zimbabwe Machi 29, lakini hadi sasa hakuna matokeo yoyote yaliyotangazwa.
Hali hiyo inaweka wasiwasi wakuweza kutokea kwa machafuko ya umwagaji damu na kuondolewa kwa madai yaliyotolewa na upande wa upinzani kuwa huenda rais Mugabe anajaribu kutaka kuiba kura ili aendelee kuwa madarakani.
Chama Tawala cha ZANU-PF kimeshindwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kiingie madarakani baada ya nchi hiyo kujipatia Uhuru kutoka kwa Mwingereza mwaka 1980 kikiwa chini ya Rais Mugabe.
Lakini wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema ushindi wa Rais Robert Mugabe utazidi kuporomosha uchumi wa nchi hiyo ambao awali ulikuwa mzuri.
Nchi za Magharibi zingependa kupeleka misaada na kuwekeza nchini humo endapo Kiongozi wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai atashinda kiti cha urais:
Morgan Tsvangira anasema yeye ndiye mshindi wa urais na anamshutumu rais Mugabe kuwa anatumia njia hiyo yakuchelewesha matokeo ili aweze kushinda kwa kisingizio cha kurudiwa kwa uchaguzi.
Naibu mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi nchini humo-ZEC, Utoile Silaigwana, amenukuliwa na Shirika la habari la Reuters akisema kuwa mpaka sasa hakuna matokeo yoyote yaliyosalia lakini anaamini kuwa yatatangazwa leo.
Wakati huohuo Mahakama Kuu nchini humo imeamuru kuachiwa huru kwa zaidi ya watu mia mbili wafuasi wa chama cha MDC waliokuwa wamefungwa jela kwa kosa la kukipigia kampeni chama hicho.