1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Goma waingiwa na hofu ya Volkano zaidi

Benjamin Kasembe27 Mei 2021

Hali ya wasiwasi imetanda katika mji wa Goma baada ya serikali ya Congo na wataalamu wa masuala ya volkeno kuomba wakaazi kuondoka kutokana na uwezekano wa mripuko mpya wa volkano kutokea

https://p.dw.com/p/3u2bQ
DR Kongo Ausbrauch Nyamulagira Vulkan
Picha: Justin Kabumba/AP Photo/picture alliance

Akitangaza kupitia redio ya taifa ,gavana wa kijeshi mkoani Kivu ya Kaskazini Constant Ndima pamoja na wataalamu wanaoshughulikia milima ya volkeno mjini Goma wametoa tangazo hilo rasmi linalo wataka wakaazi  wanaoishii katika maeneo yaliogunduliwa kuwa hatari kuondoka bila kuchelewa kufuatia uwezekano wa mripuko wa volkano na ongezeko kubwa la gesi linalo shuhudiwa katika maeneo hayo hatari.

Hata hivyo kabla ya serikali kutoa agizo hilo, maelfu ya watu  walikuwa tayari wameshaanza kuukimbia mji huu tangu siku ya Jumatano kuelekea Bukavu na Sake mbali kidogo na mji wa Goma kufuatia matetemeko ya ardhi ambayo yameendelea kuutikisa mji huu wa Goma. Asubuhi ya Alhamis kumeshuhudiwa maelfu ya wananchi wakitembea kwa mguu na wengine ndani ya magari binafsi hali ambayo inaendelea kuwatia hofu wakaazi ambao wamesalia majumbani mwao nakuamua kuanza  kukimbia .

DR Kongo Ausbrauch Nyamulagira Vulkan
Volkano katika mlima NyiragongoPicha: Steve Teril/AFP/Getty Images

Hadi tunapoenda hewani na matangazo ya mchana, hali ni ya wasiwasi katika mji huo wenye zaidi ya wakaazi milioni moja ambao wote wameanza kuyatoroka makazi yao. Hata hivyo mamlaka nchini Congo zimesema kuwa tayari magari ya umma yamewekwa ili kuwasafirisha wananchi katika vijiji vya Sake wilayani Masisi na Minova katika jimbo la Kivu Kusini.

Volkano Nyiragongo iliyo ripuka mwishoni mwa juma lililopita ,imekuwa sasa ni hatari kwa maisha ya wakaazi wa Goma ambao kulingana na vyanzo rasmi kutoka taasisi ya uchunguzi wa milima ya volkeno imedaiwa kuwa tope la volkano lenye moto limejaa ndani ya ya ardhi na uwezekano wakulipuka katika ziwa kivu.