Mkutano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi wafanyika Bonn
21 Oktoba 2015Wanadiplomasia wanaoshiriki katika mkutano huu wa Bonn wanatarajiwa kubuni muongozo utakaotumiwa na mawaziri na wakuu wa nchi kuafikiana juu ya mabadiliko ya tabianchi. Kikao cha kwanza kilikumbwa na mvutano baina ya nchi zilizostawi na zile zinanazoendelea baada ya wenye viti wa mkutano huo kutoa waraka iuliotofautiana na mapendekezo yaliyotolewa na washiriki katika mkutano wa mwezi Juni mwaka huu.
Hatua ambayo ilisababisha mvutano ulioendea karibu usiku kucha kuafikiana na matokeo yake yakawa kubuniwa kwa waraka mpya iliyojumuisha vipengee vilivyokuwa vimeachwa nje na kuongeza kurasa za waraka huo kuongezeka kutoka 20 hadi 34.
Richard Muyungi, mkurugenzi msaidizi anayehusika na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi nchini Tanzania, ni miongoni mwa wajumbe wanaohudhuria mazungumzo yanayoendelea mjini Bonn. Amesema kile kinachofanyika kwa sasa wanajaribu kupunguza muongozo huo usizidi kurasa 34.
Nchi zilizostawi zinalaumiwa na zile zinazoendelea kwa kundeleza ubagazi wakati mataifa hayo ndio yanaongoza kwa kutoa gesi chafu. Kuna hofu mvutano huo ukasababisha kujikokota kwa mazungumzo hayo. Lengo kuu la mchakato huu ni kupunguza athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza kiwango cha joto duniani kwa hadi nyuzi joto 2 kutoka kile kiwango cha sasa cha nyuzi joto 3.6.
Wanasayansi hata hivyo wasema juhudi zilizofanywa na mataifa 150 kupunguza viwango hivyo vya joto zimefikia nyuzi joto 3 pekee na kwamba ulimwengu unakabiliwa na hatari kubwa kama vile kupanda kwa kima cha maji baharini, vimbunga, ukame na kusambaa kwa magonjwa.
Mwandishi:Ambia Hirsi/AFPE/RTRE
Mhariri: Josephat Charo