1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa APC washiriki mchujo wa kumchagua mgombea urais

8 Juni 2022

Zaidi ya wajumbe 2,000 wa chama tawala cha Nigeria cha All Progressive Congress wamekusanyika katika mji mkuu Abuja kwa lengo la kumchagua mgombea atakayewania kuiongoza nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

https://p.dw.com/p/4COQ8
Nigeria Vizepräsident Yemi Osinbajo (L)
Picha: Press Office Yemi Osinbajo

Wajumbe wa chama tawala nchini Nigeria cha All Progressive Congress APC wamekutana usiku wa kuamkia leo kushiriki kura ya mchujo ya kumchagua mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao ili kuchukua nafasi ya rais Muhammadu Buhari.

Msemaji wa Buhari Garba Shehu amesema rais huyo hana mgombea anayempendelea kutoka chama hicho tawala. Wagombea waliojitokeza kuwania tiketi ya chama hicho ni pamoja na gavana wa zamani wa Lagos Bola Tinubu, Makamu wa Rais Yemi Osinbajo, waziri wa zamani wa uchukuzi Rotimi Amaechi na kiongozi wa bunge la seneti Ahmad Lawan.

Soma pia: Washambuliaji wauwa 50 kanisani Nigeria

Buhari ambaye kisheria amezuiwa kugombea tena wadhfa huo, anamaliza muhula wake mwaka 2023 baada ya miaka minane madarakani, na hivyo kusababisha uvumi juu ya mgombea atakayemuunga mkono kama mrithi wake.

Kiongozi huyo wa Nigeria aliwasili katika kituo cha mkutano cha Eagle Square mapema jana jioni kabla ya zoezi la kumchagua mrithi wake kuanza.

Buhari ametumia siku kadhaa kabla ya kongamano hilo la chama tawala akijaribu kutuma ujumbe wa umoja chamani baada ya kuibuka mirengo tofauti juu ya mgombea anayestahili kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi wa urais mnamo Februari mwakani.

Mwenyekiti wa chama hicho tawala Abdullahi Adamu, amesema, "Hatma ya chama itategemea tutakachokifanya hapa. Hatuwezi kushiriki uchaguzi mkuu mwaka ujao bila ya kuwa na umoja."

Mwenyekiti huyo amesisitiza mwito wa Buhari wa mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu. Suala ambalo limeibua mjadala mkubwa ni juu ya "kugawa maeneo"- makubaliano yasio rasmi kati ya wasomi na vigogo wa siasa kwamba Urais wa Nigeria unapaswa kupokezwa kati ya Wakristo walio wengi kutoka kusini mwa nchi hiyo na Waislamu walio wengi kutoka eneo la kaskazini.

Chama kikuu cha upinzani kimemchagua Atiku Abubakar kuwania urais

Nigeria Atiku Abubakar neuer Präsidentschaftskandidat
Aliyekuwa Makamu wa rais Atiku Abubakar amechaguliwa kuwania urais na chama cha PDPPicha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP

Baada ya Buhari ambaye ni muislamu kutoka Kaskazini mwa Nigeria kushika hatamu za uongozi, wachambuzi wa kisiasa wanataraji kuwa mgombea wa Urais safari hii atatokea upande wa kusini kwenye idadi kubwa ya Wakristo kulingana na makubaliano yasiyo rasmi ya marais waislamu na wakristo kupokezana.

Hata hivyo chama kikuu cha upinzani cha Peoples Democratic Party- PDP- ambacho kilifanya kura ya mchujo Mei 28 na 29- tayari kimemchagua makamu wa rais wa zamani Atiku Abubakar, ambaye ni muislamu kutoka Kaskazini mwa nchi hiyo kupeperusha bendera ya chama. Hatua ya upinzani kupuuza makubaliano hayo ya kupishana kati ya marais waislamu na wakristo, umekifanya chama tawala kufikiria upya juu ya mgombea wao.

Soma pia:Nigeria: Watu 168 hawajulikani walipo baada ya shambulio

Kuchaguliwa kwa Abubakar mwenye umri wa miaka 75 kunamaanisha Muislamu mwengine atakalia kiti cha Urais iwapo atashinda uchaguzi huo mnamo Februari 25, 2023.

Mkutano wa wajumbe hao wa APC mjini Abuja unafanyika siku mbili tu baada ya watu waliokuwa na silaha kuwaua kinyama waumini 22 katika kanisa kusini magharibi mwa nchi hiyo katika shambulio la risasi- na kuashiria kwamba suala la usalama litapewa kipaumbele katika uchaguzi mkuu huo.

Mgombea huyo wa urais kupitia chama tawala alitarajiwa kutangazwa mapema leo japo tangazo hilo limechelewa kutolewa.