1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajue wagombea urais katika uchaguzi wa Iran

Yusra Buwayhid
19 Mei 2017

Vituo vya kupigia kura tayari vimeshafunguliwa nchini Iran na raia wa nchi hiyo wanachagua rais wao mpya. Lakini ni nani wagombea wakuu wanaopigania nafasi ya urais katika uchaguzi wa leo?

https://p.dw.com/p/2dDt0
Iran wahlen 2017
Picha: Mehr

Kuchaguliwa tena au kutochaguliwa kwa rais wa sasa Hassan Rouhani kunaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa sio tu za ndani ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu, bali pia kimataifa, kwani uchaguzi huu unaweza kwa kiasi kikubwa kuathiri mustakbali wa baadaye wa nchi hiyo.

Takriban vituo vya kupigia kura 63,000 vimefunguliwa leo hii kuanzia saa mbili asubuhi, nchini kote. Hata hivyo, kutokana na kuwepo watu milioni 54 walio na haki ya kupiga kura, pamoja na kuwepo kawaida ya wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura, matokeo ya awali hayatarajiwi kutolewa hadi Jumamosi.

Uwezo wa Iran wa silaha za kinyuklia na umuhimu wa kimkakati ulio nao nchi hiyo katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, ni masuala mawili makuu yanayozingatiwa wakati wa kupiga kura leo hii.

Wapiga kura nchini humo wataweza kuchagua miongoni mwa wagombea wanne.

Iran Präsident Rohani zu U.S. Luftschlägen gegen syrischen Luftwaffenstützpunkt
Rais aliyepo madarakani Hassan RouhaniPicha: picture-alliance/AA/Iranian Presidency

Kwanza ni Hassan Rouhani msomi wa kidini na mwanasheria mwenye umri wa miaka 68 na ndiye rais aliyepo madarakani kwa sasa. Rouhani anatazamwa kama mwanamageuzi wa misimamo ya wastani, na ni mmoja wa wagombea wawili wanaongoza katika kinyang'anyiro hicho cha urais akifuatiwa na Ebrahim Raisi.

Wakati wa muhula wake wa kwanza Rouhani, alifungua milango ya nchi hiyo na kuzikaribisha nchi za Magharibi, alisimamia makubaliano ya 2015 ambayo yaliihitaji Iran kupunguza uwezo wake wa kinyuklia, ili nchi za Magharibi kwa upande wake zipunguze vikwazo vya kimataifa ilivyoiwekea nchi hiyo. Rouhani ameahidi kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia na amesema ataendelea na kazi ya kuvutia zaidi uwekezaji wa kimataifa nchini Iran iwapo atachaguliwa tena.

Iran Präsidentschaftswahl | Ebrahim Raisi
Mgombea urais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Reuters/Tima

Mgombea wa pili ni Ebrahim Raisi, kiongozi wa kidini mwenye umri wa miaka 57 ambaye anatazamwa kama mshirika wa karibu na anayeweza kumpokea madaraka Kiongozi Mkuu wa Kidini, Ali Khamenei.

Ingawa Raisi hataki kusitisha makubaliano ya kinyuklia yaliyofikiwa mwaka 2015, lakini amesema Iran inapaswa kujitenga kisiasa na kiuchumi kutoka nchi za Magharibi. Raisi pia anapinga uwekezaji zaidi wa kigeni.

Iran Präsidentschaftswahl | Mostafa Mirsalim
Mgombea urais katika uchaguzi wa Iran Mostafa MirsalimPicha: Reuters/Tasnim

Mostafa Mirsalim ni mgombea mwengine wa tatu ambaye aliwahi kuwa waziri wa utamaduni na anatazamwa kama mtu mwenye misimamo mikali ya kihafidhina. Nafasi yake ya kushinda katika uchaguzi huu inatarajiwa kuwa ni ndogo sana.

Na mgombea wa nne katika uchaguzi wa leo wa rais unaofanyika nchini Iran ni Mostafa Hashemitaba. Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 76 na mwenye misiamamo ya kisiasa ya wastani aliwahi kuwa makamu wa rais kuanzia 1997 - 2005 chini ya uongozi wa Mohammad Khatami, mwanamageuzi wa kwanza kuwahi kuwa rais nchini humo.

Iran Präsidentschaftswahl | Mostafa Hashemitaba
Mgombea urais wa Iran Mostafa HashemitabaPicha: picture-alliance/AP Photo

Uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Iran na nchi za Magharibi kama vile Marekani pamoja na nchi jirani Saudi Arabia, ambayo ni msaidizi muhimu wa makundi ya waasi ya nchini Syria, unaweza kurahisisha mazungumzo ya amani siku za baadaye.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/DW

Mhariri: Mohammed Khelef