Wajue waandishi walioteswa kwa kazi zao
Kila mwaka Novemba 15, PEN International inasimulia visa vya waandishi watano ambao walinyanyaswa kwa kazi zao. Mwaka huu wanakumbukwa Lydia Cacho, Stella Nyanzi, Nedim Türfent, Galal El-Behairy na Shakthika Sathkumara.
Lydia Cacho Ribeiro, Mexico
Mwandishi mashuhuri wa uchunguzi wa Mexico na mwanaharakati amekumbana na unyanyasaji, shambulio na vitisho vya kifo kwa muda mrefu. Alishikiliwa kizuizini kiharamu mwaka 2005 baada ya kutoa kitabu kilichoangazia mitandao ya ukahaba wa watoto. Aliposhambuliwa nyumbani kwake Julai 2019, vifaa vyake vya uchunguzi viliibiwa na mbwa wake waliuawa. Tukio hilo lilimlazimisha kuhamia uhamishoni.
Shakthika Sathkumara, Sri Lanka
Mwandishi aliyeshinda tuzo ya mwandishi wa Sri Lanka, Shakthika Sathkumara aliandika kwenye Facebook moja ya hadithi fupi fupi zilizogusia unyanyasaji wa watoto kwenye hekalu la Wabudha. Alishutumiwa kwa kuchochea chuki za kidini. Tayari alikuwa kizuizini kwa zaidi ya siku 120 wakati akichunguzwa na polisi. Anakabiliwa na kifungo cha miaka 10 ikiwa atakuwa na hatia katika kesi ya mwezi Disemba.
Stella Nyanzi, Uganda
Uganda imekuwa ikiwachukulia hatua kali wakosoaji wa mitandaoni. Mfano mzuri wa hii ni kesi ya msomi, mwandishi na mwanaharakati Stella Nyanzi. Mnamo Septemba 2018, alichapisha shairi kwenye Facebook lililomkosoa rais wa nchi hiyo na mama yake. Agosti mwaka huu alihukumiwa kifungo cha jela hadi miezi 18 kwa "udhalilishaji wa mtandaoni."
Nedim Turfent, Uturuki.
Nedim Turfent alikamatwa mnamo Mei 2016 kufuatia ripoti yake kuhusu mapigano ya jeshi katika eneo la Kikurdi la Uturuki. Alishtakiwa kwa ugaidi, alihukumiwa kifungo cha karibu miaka tisa lakini ilimbidi atumie karibu miaka miwili kizuizini. Walakini, kesi ya mwandishi huyo haikuwa ya haki; Mashuhuda 19 baadaye walisema waliteswa ili kutoa ushuhuda dhidi yake.
Galal El-Behairy, Misri.
Mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa rais wa Misri, wimbo uliokuwa na mashairi yaliyoandikwa na Galal El-Behairy kukosoa serikali yalisambaa nchini humo. Hiyo ilimfanya waziri wa utamaduni wa Misri kulaani mashairi yaliyokuwa kwenye kitabu chake cha "Wanawake Wazuri zaidi Duniani." Mwandhishi huyo baadaye alikamatwa na kuteswa. Anatumikia kifungo cha miaka 3 katika moja ya magereza mashuhuri ya Misri.