Tanzania inamsubiri rais wa awamu ya tano
26 Oktoba 2015Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyezaliwa Butiama, wilaya ya Musoma, mkoani Mara, Mnamo tarehe 13 Aprili 1922 alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania na ndiye ajulikanaye kuwa baba wa Taifa la Tanzania.
Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia mnamo tarehe 14 mwezi Oktoba mwaka 1999 ndiye muanzilishi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea iliyotangazwa hasa katika Azimio la Arusha.
Kabla ya kujitosa katika masuala ya kisiasa alikuwa ni mwalimu, tasnia ambayo ilimpa jina ambalo alitambulika nalo kote duniani Mwalimu.
Kiongozi huyo aliiongoza Tanganyika toka mwaka 1961 hadi 1964 kama waziri mkuu, kisha baadaye kama Rais baada ya muungano Wa Tanganyika na Zanzibar, aliongoza Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1985 kama rais.
Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954 alibadilisha jina la chama cha TAA kwenda chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika.
Uwezo wa Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akijisemea kuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.
Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la udhamini na Kamati ya nne ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.
Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
Tarehe 5 Februari 1977 aliongoza chama cha TANU kuungana na chama tawala cha Zanzibar Afro Shirazi Party na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa mwenyekiti wake wa kwanza.
Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiari baada ya kutawala kwa muda mrefu akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi.
Alipostaafu urais mwaka 1985 na kumpisha Ali Hassan Mwinyi kuliongoza taifa la Tanzania, alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Hata hivyo aliendelea kuongoza CCM hadi mwaka 1990 na kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Kati ya mafanikio makubwa ya Nyerere kuna: kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi jirani, iliyofanya Tanzania iitwe "kisiwa cha amani".
Pia kustawisha utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, kutetea usalama wa taifa katika vita dhidi ya mvamizi Idi Amin wa Uganda.
Kutoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile Zimbabwe Afrika Kusini , Namibia, Angola na Msumbiji.
Kila jema msikilzaji bila shaka pia halikosi kasoro-Nyerere analaumiwa kwa siasa yake ya kiujamaa kuwa ilichelewesha maendeleo ya kiuchumi wa Tanzania.
Kuna walio na mtizamo Nyerere alimhadaa aliyekuwa Rais wa Zanzibar Mzee Abeid Amaan Karume kwa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar, na kuanza kupora mamlaka ya Zanzibar kidogo kidogo.
Licha ya hayo, Hayati Mwalimu Nyerere bado anakumbukwa na Watanzania wengi kutokana na sera zake za kujali utu. Pia ataendelea kukumbukwa na barabi Afrika kwa mchango wake katika harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika. Ni mmoja wa viongozi wachache kutoka Afrika wanaoheshimika duniani kwa uadilifu kwa kutojilimbikizia mali na kuachia madaraka kwa hiari.
Ali Hassan Mwinyi:
Ali Hassan Mwinyi alikuwa Rais wa Pili wa Tanzania kuanzia 1985 hadi 1995. Kabla ya kuchaguliwa kuliongoza taifa hilo, Mwinyi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamu wa Rais. Vile vile alishikilia wadhifa wa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia 1990 hadi 1996.
Mwinyi aliyezaliwa kwenye kisiwa cha Unguja Zanzibar,wakati wa utawala wake, sera za Ujamaa zilianza kugeuzwa. Badala yake sera za soko huru zilianzishwa, masharti ya kuingiza bidhaa kutoka nchi za nje yalipunguzwa na uanzishaji wa biashara za watu binafsi ulihimizwa Ni wakati wa utawala wake, Mwaka wa 1991, mchakato wa kuanzisha siasa za vyama vingi iliruhusiwa Tanzania. Mwinyi baada ya kustaafu mwaka 1995 hakujiingiza katika mambo ya siasa tena. Anaendelea kuishi huko Dar es Salaam.
Benjamin Mkapa:
Mwaka wa 1995, Benjamini William Mkapa aliyezaliwa tarehe 12 Novemba 1938 alichaguliwa rais msingi wake ukiwa kwa kampeni maarufu ya kupambana na ufisadi na kwa kumuunga mkono kwa nguvu rais wa zamani Julius Nyerere .
Juhudi za Mkapa za kupambana na ufisadi ni pamoja na kuundwa kwa jukwaa la wazi lililoitwa Tume ya Rais juu ya Ufisadi (Tume ya Warioba) na kuongeza msaada kwa Afisi ya Kuzuia Ufisadi.
Katika wakati wake madarakani, Mkapa alibinafsisha makampuni yanayomilikiwa na serikali na akaweka sera za soko huru. Sera zake zilipata msaada wa Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani IMF na kupelekea baadhi ya madeni ya nje ya Tanzania kufutiliwa mbali.
Mkapa aliondoka madarakani mwaka 2005 baada ya kukamilisha muhula wa pili kuambatana na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Jakaya Mrisho Kikwete:
Rais wa sasa wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyezaliwa tarehe 7 Oktoba mwaka 1950 Msoga, mkoa wa Pwani.
Mwaka 1988 aliteuliwa kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Mwaka 1990 alichaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Bagamoyo na akateuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini.
Nyadhifa nyingine alizoshika ni Waziri wa Fedha mwaka 1994 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005. Alishika rasmi wadhifa wa urais mwaka 2005 na kuchaguliwa tena 2010 kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Anaondoka madarakani baada ya uchaguzi huu wa 2015 baada ya kuhudumu mihula miwili. Sasa kinachosubiriwa ni je nani atakuwa Rais ajaye madarakani? atasimamia misingi ipi na ajenda zake kwa watanzania zitakuwa ni zipi? Hilo tutalijua ndani ya kipindi cha wiki hii.
Mwandishi: Caro Robi
Mhariri: Iddi Ssessanga