1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wapiga kura, Merkel apania awamu ya tatu

Josephat Nyiro Charo22 Septemba 2013

Wajerumani wamepiga kura leo katika uchaguzi mkuu ambao yumkini ukampa ushindi kansela Angela Merkel na kuingoza Ujerumani kwa awamu ya tatu, ingawa huenda akalazimika kutawala na wapinzani wake wakuu.

https://p.dw.com/p/19lys
German Chancellor Angela Merkel poses as she casts her ballot during the German general election (Bundestagswahl) at a polling station in Berlin, September 22, 2013. The person at left is Merkel's husband Joachim Sauer. REUTERS/Kai Pfaffenbach (GERMANY - Tags: POLITICS ELECTIONS) ***FREI FÜR SOCIAL MEDIA***
Angela Merkel alipopiga kura BerlinPicha: Reuters

Kura za maoni zinaashiria kwamba wapigaji kura watamchagua Bi Merkel, mtoto wa kike wa mchungaji kutoka Ujerumani Mashariki, ambaye hujulikana kwa jina la utani kama "Mutti" - yaani mama. Kansela Merkel amepiga kura katika kituo cha kupigia kura kilichoko chuo kikuu cha Humboldt mjini Berlin pamoja na mumewe, Joachim Sauer. Merkel analazimika kupiga kura katika jimbo la Berlin anakoishi, lakini anagombea kuchaguliwa katika jimbo lengine la kaskazini mwa Berlin, ambalo amekuwa alikiwakilisha bungeni tangu mwaka 1990.

Kauli tofauti za wapiga kura

Wapigaji kura walitiririka katika mgawa wa chuo hicho kutumbukiza kura zao. "Nadhani tuna kiwango kizuri cha maisha barani Ulaya na kwangu mimi, kiwango hiki kinatakiwa kubakia imara. Kwa hiyo kwa mimi kupigia kura viongozi wa mrengo wa kulia au shoto, si jawabu," amesema Elisabeth Bauer, wakati alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Marissa Kutscha, mwenye umri wa miaka 26, amekiri umekuwa na wakati mgumu. "Sikuwa na uhakika nimpigie kura nani au chama gani, kwa sababu hakuna tofauti kubwa sana kati ya vyama."

"Nimekipigia kura chama cha Christian Democratic, CDU, kwa sababu ni chama ambacho kimeonyesha nia ya kuipeleke nchi mbele katika miaka minane iliyopita," amesema Jochen Anders, afisa wa polisi mwenye umri wa miaka 58 baada ya kupiga kura mjini Berlin.

"Tunaendelea vyema hapa Ujerumani, hatuhitaji mabadiliko yoyote", amesema Herbert Wedrich, muuzaji bidhaa katika duka mwenye umri wa miaka 64 baada ya kutumbukiza kura yake katika mji wa Frankfurt.

Wapiga kura wengi wajitokeza

Wapiga kura milioni 62 wana haki ya kupiga kura. Maafisa wa uchaguzi wamesema kufikia mwendo wa saa nane mchana asilimia 41.4 ya wapiga kura walikuwa wamejitokeza, ikiashiria kwamba idadi jumla ya wapigaji kura watakaoshiriki katika zoezi la kupiga kura huenda ikawa juu ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.

Mnamo mwaka 2009, asilimia 36.1 ya wapigaji kura walikuwa wameshatumbukiza kura zao kufikia saa sita mchana katika uchaguzi wa bunge. Hata hivyo takwimu zilizotolewa na maafisa wa uchaguzi hazijumuishi kura zilizopigwa kwa njia ya posta, mfumo ambao katika uchaguzi huu umepata umaarufu mkubwa.

BONN, GERMANY - SEPTEMBER 22: Peer Steinbrueck, chancellor candidate of the German Social Democrats (SPD) casts his ballot in German federal elections on September 22, 2013 in Bonn, Germany. Germany is holding federal elections that will determine whether current Chancellor Angela Merkel of the German Christian Democrats (CDU) will remain for a third term. Though the CDU has a strong lead over the opposition, speculations run wide as to what coalition will be viable in coming weeks to create a new government. (Photo by Dennis Grombkowski/Getty Images)
Peer SteinbrückPicha: Getty Images

Mpinzani mkuu wa Merkel katika uchaguzi wa leo, Peer Steinbrück, alipiga kura na mkewe katika mji anakotokea wa Bonn. "Leo ni siku ya uchaguzi. Mustakabali wa taifa hili uko mikononi mwenu. Tafadhalini nendeni mkapige kura," amesema Steinbrück kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter mapema leo.

Bara la Ulaya linauangalia kwa karibu uchaguzi wa Ujerumani ambao ni wa kwanza tangu kutokea msukosuko wa kiuchumi mnamo mwaka 2009 ulioikumba dunia. Baadhi wana matumaini Merkel atalegeza msimamo wake kuhusu mataifa yanayoyumba kiichumi katika kanda inayotumia sarafu ya euro kama vile Ugiriki, kama atalazimika kuunda serikali ya mseto na chama cha upinzani cha Social Democratic, SPD

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman