1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wagawika kuhusu muhula wa nne kwa Merkel

28 Agosti 2016

Uchunguzi mpya wa maoni umegunduwa Wajerumani wamegawika kuhusiana na suala iwapo Kansela Angela Merkel awanie muhula wa nne madarakani ambapo wengi wanamshutumu kwa sera yake ya kukaribisha wakimbizi nchini.

https://p.dw.com/p/1JrJe
Picha: picture-alliance/dpa/T. Carmus

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliochapishwa Jumapili (28.08.2016) na gazeti la Ujerumani la "Bild am Sonntag" umashuhuri wa Merkel nchini umeshuka ambapo asilimia hamsini wanapinga kutumikia muhula wa nne madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mlolongo wa mashambulizi ya matumizi ya nguvu dhidi ya raia hapo mwezi wa Julai ambapo mawili kati yao yalidaiwa kuwa na mkono wa kundi la Dola la Kiislamu yameliweka upenuni suala la sera ya Merkel ya kuwafungulia milango wahamiaji ambayo imewaruhusu mamia kwa maelfu ya wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati, Afrika na kwengineko kuingia Ujerumani mwaka jana.

Nusu ya watu 501 waliohojiwa na kampuni ya Emnid iliofanya uchunguzi huo wa maoni kwa niaba ya gazeti hilo la Ujerumani wasingependa kuona Merkel anaendelea kubakia madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 wakati asilimia 42 wakitaka aendelee kubakia.Merkel amekuwa akishutumiwa na raia pamoja na wanasiasa wenzake kutokana na sera zake hizo za wakimbizi.

Alipoulizwa kuhusu mipango yake kwa uchaguzi mwa mwaka 2017 na gazeti la kimkoa lililochapishwa hapo Jumanne Merkel amesema : "Nitalizungumzia hilo wakati utakapofika na nashikilia msimamo huo." Hadi sasa Merkel anatarajiwa kutangaza uamuzi wake wakati wa kipindi cha majira ya machipuko mwakani.

Kushuka kwa umashuhuri wa Merkel

Hapo mwezi wa Novemba mara ya mwisho wa gazeti hilo la Bild am Sonntag kuagiza kufanyiwa uchunguzi huo wa maoni asilimia 45 walikuwa wakipendelea Merkel aendelee kubakia madarakani kwa muhula wa nne wakati waliopinga walikuwa asilimia 48.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Asilimia 70 ya wafuasi wake ndani ya chama chake cha kihafidhina cha Christian Demokratik (CDU) wanaunga mkono muhula mwengine kwa Merkel wakati asilimia 22 wakipinga.

Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani la "Der Spiegel " Merkel ambaye hakutangaza iwapo atawania muhula huo wa nne au la anasubiri kuona iwapo ataungwa mkono na chama ndugu cha Christian Social Union (CSU) cha jimbo la Bavaria.

Iwapo Merkel atashinda muhula mwengine anaweza kuweka rrekodi mpya ya kuwa kansela aliekaa madarakani kwa muda mrefu kabisa .Rekodi ya sasa inashikiliwa na Helmut Kohl ambaye aliushikilia wadhifa huo kwa miaka 16 tokea mwaka 1982 hadi mwaka 1998.

Uchaguzi mpya wa Ujerumani unatarajiwa kufanyika kati ya Agusti 27 na Oktoba 22 mwaka 2017. Merkel alichaguliwa kuwa Kansela hapo mwezi wa Novemba mwaka 2005 na hivi sasa anatumikia muhula wake wa tatu.

CDU haikujiandaa kwa changamoto

Merkel anaongoza serikali ya muungano mkuu kwa kushirikiana na chama cha CSU na chama cha sera za mrengo wa wastani kushoto cha Social Demokratik Union (SPD).

Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel wa chama cha SPD.
Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel wa chama cha SPD.Picha: picture alliance/dpa/E. Wabitsch

Hata hivyo mvutano umekuwa ukiongezeka kwenye serikali hiyo ya muungano kutokana na sera za Merkel za wahamiaji na kujumuishwa katika jamii kukabiliana na wimbi kubwa la watafuta hifadhi nchini hapo mwaka jana.

Naibu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema hapo Jumamosi kwamba chama cha Mekel cha CDU kimekadiria vibaya changamoto za kuwajumuisha katika jamii ya Ujerumani wahamiaji wapya wanaowasili.

Pia ameikosowa kauli mbi ya Merkel "Wir schaffen das" Tunalimudu hili ambayo amekuwa akiitumia mara kwa mara katika kugusia suala la kuushughulikia mzozo wa wahamiaji.Gabriel amesema kwa kurudia neno haitoshi kuutatuws mzozo huo bila ya chama hicho cha CDU kuanzisha mazingira zaidi kuwawezesha Wajerumani waweze kukabiliana na hali hiyo.

Idadi ya wakimbizi ni ndogo

Juu ya kwamba makadirio ya awali yalisema Ujerumani ilipokea takriban wahamiaji na wakimbizi milioni moja nukta moja mwaka jana maafisa hivi sasa wanasema kwa kweli idadi ni ndogo kuliko hiyo.

Wakimbizi wakishiriki mafunzo ya lugha ya Kijerumani.
Wakimbizi wakishiriki mafunzo ya lugha ya Kijerumani.Picha: Getty Images/C. Koall

Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumapili na gazeti la "Bild am Sonntag" mkuu wa ofisi ya Wahamiaji na Wakimbizi katika serikali ya Ujerumani (BAMF) amesema usajili uliofanyika mara mbili na wale walioendelea na safari kutoka Ujerumani kwenda nchi nyengine yamefanya mahesabu kuwa makubwa kwa makosa.

Frank -Jürgen Weise ameliambia gazeti hilo "Kilicho na uhakika ni kwamba mwaka jana watu walioingia nchini Ujerumani walikuwa chini ya milioni moja na kwamba marekebisho ya mahesabu hayo yatawasilishwa hivi karibuni.

Kiongozi huo wa BAMF amesema ofisi yake ilikuwa ikitarajia kuwasili kwa wahamiaji wapya mwaka huu kati ya 250,000 na 300,000 idadi ambayo ni tafauti kabisa na ile ya waliowasili mwaka jana.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : Yusra Buwayhid