Wajerumani wagawanyika kuhusu wahamiaji
7 Septemba 2018Mjadala huo unaohusiana na hatua ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kufungua milango kwa ajili ya wahamiaji umeibuliwa tena wiki iliyopita baada ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia kuandamana kufuatia kuchomwa kisu mwanaume mjerumani mwenye umri wa miaka 35 August 26 katika mji wa mashariki wa Chemnitz . Wanaume wawili mmoja raia wa Iraq na mwingine wa Syria wametiwa mbaroni wakihusishwa na shambulizi hilo.
Hata hivyo maandamano hayo yalijibiwa haraka na kundi lingine la waandamanaji waliokuwa wakiyapinga.
Hayo yanajiri mnamo wakati mkuu wa shirika la ujasusi wa ndani nchini Ujerumani Hans Georg Maassen akionesha mashaka kuhusiana na taarifa zinazodai kwamba wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia walikuwa wakiwakimbiza wageni wakati wa maandamano yaliyofanyika katika mji huo wa Chemnitz, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa gazeti la Bild katika taarifa yake leo Ijumaa.
Akitolea mfano wa vidio inayosambaa mtandaoni inayoonesha wafuasi wa mrengo wa kulia wakiwafukuza watu walioonekana kuwa sio wajerumani, Maassen alisema hakuna ushahidi unaodhihirisha kuwa vidio hiyo ni ya kweli.
Ameongeza kuwa idara yake inayohusika na kulinda katiba haina taarifa kuwa kitendo kama hicho kilifanyika na kusisitiza kuwa kuna sababu za msingi za kuamini kuwa habari hizo zilikuwa za upotoshaji wa makusudi za kuufanya umma uache kufuatilia kisa cha mauaji ya mjini mjini Chemnitz.
Raia kadhaa wa mataifa yakigeni wadai kuandamwa
Wakati wa maandamano ya awali August 26 mwandishi mmoja wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Die Zeit alichapisha vidio mbili mtandaoni zikionesha waandamanaji wakiwafukuza watu wanaonekana kuwa na asili ya kigeni. Polisi wanasema watu kadhaa wakiwemo wabulgaria,wasyria na waafghanistan walidai walivamiwa na waandamanaji.
Hivi karibuni Maassen alibanwa kufuatia mkutano wake na wafuasi wa chama kinachopinga wahamiaji nchini Ujerumani chama mbadala kwa ujerumani (AfD).
Kitabu kilichoandikwa na mmoja wa wanachama wa zamani wa chama cha AfD kinadai kuwa katika moja ya mikutano hiyo iliyomshirikisha mwenyekiti wa zamani wa chama cha AfD Frauke Petry, Maassen aligusia jinsi ya kukwepa kufuatiliwa na shirika la ujasusi wa ndani nchini Ujerumani.
Aidha waziri mkuu wa serikali ya jimbo la Saxony, Michael Kretschmer amesema pia kuwa maandamano hayo ya wafuasi wa mrengo wa kulia hayakuwa dhidi ya wahamiaji.
Hata hivyo kauli hiyo inakinzana na matamshi yaliyotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anayesema kuwa vidio inayosambaa mtandaoni inaonesha jinsi maandamano hayo yalivyolenga kuonesha chuki dhidi ya wageni na kusisitiza kuwa vitendo hivyo havina nafasi chini ya utawala wa sheria.
Mshukiwa wa tatu katika mauaji hayo dhidi ya mwanaume wa Kijerumani mjini Chemnitz bado anatafutwa.
Mwandishi: Isaac Gamba /Dw
Mhariri : Gakuba, Daniel