Wajapan waandamana Yokohama
13 Novemba 2010Kiasi Wajapan 4,000 wameandamana katika mji wa Yokohama kupinga ziara ya Rais wa China, Hu Jintao anayehudhuria mkutano wa kiuchumi wa mataifa ya Asia na eneo la Pacific-APEC.
Viongozi kutoka nchi 21 wa nchi za APEC wanakutana mjini Yokohama, Japan kwa ajili ya mkutano wa mwaka wa umoja huo, kuhusu ushirikiano wa kiuchumi.
Waandamanaji hao wanaimba nyimbo zenye maneno yanayozungumzia ubeberu wa China, wakitilia mkazo mzozo wa China na Japan kuhusu visiwa vilivyoko katika Bahari ya China Mashariki.
Pamoja na mambo mengine, Rais Barack Obama wa Marekani, Hu Jintao na viongozi wengine wa APEC, wanatarajiwa kujadili kuhusu masuala ya nishati na kuchukua hatua kuelekea kuanzisha eneo pana la biashara huria katika eneo la Pacific.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AP,AFP)
Mhariri: Mohamed Dahman