Waislamu waanza mwezi mtukufu wa Ramadhan
1 Septemba 2008Waislamu takriban wote duniani wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan ambapo wanatakiwa kujizuia kula na kunywa na kujiepusha na starehe za aina yoyote kuanzia macheo hadi machweo kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Katika ukanda wa Gaza wakaazi wanazidi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kuendelea kuwepo vizuizi vya Israel licha ya taifa hilo kufikia makubaliano ya kusitisha vita na wanamgambo wakipalestina wanaodhibiti eneo hilo.
Vizuizi vya Israeli Ukanda wa Gaza vimesabisha ukosefu wa vyakula,mafuta pamoja na mahitaji mengine muhimu.
Nchini Somalia kabla ya kuanza kwa mwezi wa Ramadan mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa anayehusika na misaada ya kiutu Abdul Aziz Arrukban alitoa mwito kwa jamii ya kimataifa na hasa nchi za kiislamu kuongeza misaada katika nchi hiyo inayokabiliwa na mzozo.
Maeneo mengi ya Somalia yanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa vyakula ambapo kwa mujibu wa Umoja huo wa mataifa watu zaidi ya millioni tatu wanahitaji haraka msaada wa chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu.
Kwa upande mwingine serikali ya Pakistan imesimamisha oprehsheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo huko kaskazini mashariki mwa nchi kufuatia kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhan.Baadhi ya waislamu wanatarajiwa kuanza mfungo huo wa ramadhan hapo Kesho jumanne.