1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu waanza kusherehekea Eid ul Fitri

Admin.WagnerD8 Agosti 2013

Waislamu katika baadhi ya mataifa ulimwenguni wanaadhimisha siku kuu ya Eid ul Fitr hii leo, huku wengine wakitarajiwa kusherehekea sikukuu hiyo siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/19LyR
Muslims perform Eid al-Adha prayers at the Jama Masjid in the old quarters of Delhi October 27, 2012. Muslims around the world celebrate Eid-al-Adha, marking the end of the haj, by slaughtering sheep, goats, cows and camels to commemorate Prophet Abraham's willingness to sacrifice his son Ismail on God's command. REUTERS/B Mathur (INDIA - Tags: RELIGION TPX IMAGES OF THE DAY)
Bildergalerie Muslimisches Opferfest Eid al Adha 2012Picha: Reuters

Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Misri ni miongoni mwa mataifa ya Kiislamu ambako mamilioni ya waumini wamefurika misikitini asubuhi ya leo kuhudhuria swala iliyofanyika majira ya asubuhi na kisha kufuatiwa na sherehe za Eid al-Fitr, zinazohitimisha mwezi mzima wa kufunga kuanzia alfajir hadi kuzama kwa jua, wakijizuia kula, kunywa, kuvuta na mengine yanayobatilisha saumu zao kama njia ya kuijaribu imani yao. Siku ya Eid pia ni wakati wa kutafakari, kusamehe na kufanya hisani.

Waislamu wakipongezana kufuatia kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Waislamu wakipongezana kufuatia kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.Picha: Romeo Gacad/AFP/Getty Images

Tanzania, Kenya Ijumaa
Lakini si mataifa yote yanaanza sherehe hizi kwa wakati mmoja. Tanzania na Kenya kwa mfano zinatarajia kuanza rasmi sherehe za Eid kesho Ijumaa, baada ya maafisa katika nchi hizo kutofanikiwa kuuona mwezi hapo jana. Na licha ya ujumbe wa amani wa siku ya Eid, baadhi ya nchi zimeendelea kuwa katika hali y atahadhari kubwa kutokana na wasiwasi wa kutokea kwa vurugu.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mwandishi wa DW mjini Kinshasa Saleh Mwanamilongo ameripoti kuwa Waislamu nchini humo wameswali swala ya Eid chini ya alama ya mshikamano na ndugu zao walioko vitani mashariki mwa nchi hiyo, wakati wengine wamemaliza funga katika mazingira magumu kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na mfumko wa bei.

Waziri Westerwelle awapongeza Waislamu
Katika ujumbe wake wa siku ya Eid ul Fitr, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Dokta Guido Westerwelle, amewatakia Waislamu duniani kote heri ya siku kuu hii, na kusema kuwa wakati wa kumaliza mwezi wa Ramadhani ni wakati wa kufurahia, kushiriki pamoja na kuonyesha upendo kwa wengine.

Hata hivyo, Waziri Westerwelle aliezea masikitiko juu ya ukweli kwamba baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali ya dunia hawakuweza kusherehekea siku kuu hii kwa amani kwa sababu za vurugu, huku wengine wakipoteza maisha yao na wengine wakilaazimika kuwa wakimbizi kutokana na vita vinavyoendelea katika mataifa yao. Alisema ni muhimu kwa wakati huu kuendeleza majadiliano na kufanya kazi kwa pamoja kati ya watu wa dini mbalimbali ili kuendelea kuishi kwa amani na upendo nchini Ujerumani na duniani kote.

Nchini Afghanistan, swala yafanyika chini ya ulinzi mkali.
Nchini Afghanistan, swala yafanyika chini ya ulinzi mkali.Picha: Aref Karimi/AFP/Getty Images

Khofu ya mashambulizi ya kigaidi
Wasiwasi ulitanda katika baadhi ya mataifa ya mashariki ya kati na Afrika, baada ya Marekani kufunga kwa muda vituo vyake 19 vya kidiplomasia kufuatia wasiwasi wa kutokea mashambulizi ya kigaidi, huku nchi hiyo na Uingereza zikiondoa wafanyakazi wake katika balozi zao nchini Yemen, ambako serikali ilisema kuwa imezuia njama ya kundi la Al-Qaeda.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu aliteremsha aya za kwanza za Qur-an Tukufu kwa Mtume Muhammad S.A.W wakati wa mwezi wa Ramadhani, ambao unaanza kwa kuandama kwa mwezi mpya. Kalenda ya Kiislamu inabadilika mara kwa mara, na hii inamaanisha kuwa Ramadhani inaanza siku 11 mapema kila mwaka chini ya kalenda ya kimagharibi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef