1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu waadhimisha Idd-al-Fitr

Mohammed Khelef6 Julai 2016

Waislamu ulimwenguni kote wanaadhimisha sikukuu ya Idd-al-Fitr kufuatia kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, moja ya nguzo tano muhimu za Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1JJy4
Waislamu wakisherehekea Idd-al-Fitr mjini Jakarta, Indonesia.
Waislamu wakisherehekea Idd-al-Fitr mjini Jakarta, Indonesia.Picha: Getty Images/U. Ifansasti
Kutoka mashariki hadi magharibi, kaskazini hadi kusini, leo ni siku inayotukuzwa na umma wa waumini bilioni 1.6 duniani kote. Maelfu ya waumini walijitokeza misikitini majira ya saa moja asubuhi ya leo nchini Indonesia, taifa la Asia Kusini na linalotambulika kuwa na Waislamu wengi zaidi duniani.
Sala hiyo iliendeshwa pia kwenye viwanja vya wazi katika maeneo mbalimbali ya Afrika ya Mashariki, kuanzia Comoro hadi Zanzibar, Nairobi hadi Kigali, Kampala hadi Bujumbura.
Nchini Afghanistan, Rais Ashraf Ghani katika salamu zake za sikukuu alitoa wito wa amani kwa taifa hilo linaloendelea kupitia vipindi vigumu vya vita. "Ninatuma salamu zangu za Eid al-Fitr kwa taifa tukufu la Afghanistan na ndugu zetu wa Kiislamu kote duniani." Alisema kiongozi huyo, akiongeza kwamba akiwa kama mkuu wa serikali yenye dhamana ya kusaka na kusimamia amani, daima anatazamia amani kuwapo kwa watu wote.
Katika ardhi inayokaliwa huko Ukingo wa Magharibi, Wapalestina wamejitokeza kwa wingi kuadhimisha sikukuu hii kwenye viunga vya wilaya ya Hebron, huku wakitoa wito kwa Israel kuondosha vizuizi vya barabarani, angalau kuwapa nafasi ya kusherehekea kwa nafasi.
Siku ya Ijumaa, Israel ilituma mamia ya wanajeshi wake kwenye wilaya hiyo, kufuatia wimbi la mashambulizi dhidi ya raia wake kwenye upande wa kusini wa Ukingo wa Magharibi.
Mama na mwanawe kwenye sherehe za Idd-al-Fitr nchini Algeria.
Mama na mwanawe kwenye sherehe za Idd-al-Fitr nchini Algeria.Picha: DW
Nchini Iraq, maelfu ya waumini walikusanyika kwenye msikiti wa Imamu al-Khalani katika mji mkuu Baghdad, licha ya wasiwasi kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama. Katika hotuba yake, imamu wa msikiti huo mashuhuri, Sheikh Salih al-Haydari, alilaani mauaji dhidi ya vikongwe, wanawake na watoto yanayofanywa na makundi ya kihalifu yakitumia mgongo wa dini.

Sheikh al-Haydari ameyataja makundi hayo kama maadui wa umma wa Kiislamu duniani kote, na kuitaka serikali kuwaandama vilivyo. Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, linasema limehusika na mauaji ya watu 200 kufuatia mashambulizi ya hapo Julai 3 mjini Baghdad.

Nchini Syria, taifa ambalo pia linakabiliwa na ukatili mkubwa wa kundi hilo na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya waasi na serikali, Rais Bashar al-Assad alijitokeza hadharani katika kitongoji cha Akrama, kwenye mji mkuu Damascus, kwa Sala ya Idd.
Assad ameonekana kwenye msikiti wa al-Safa akiambatana na waziri wake wa masuala ya Kiislamu, Mohammed Abdel-Sattar na mufti mkuu Ahmad Badruddin Hassouni. Muda mfupi baadaye, shirika la utangazaji la nchi hiyo, lilitangaza masaa 72 ya kusitishwa mapigano kwa heshima ya sikukuu.

Eid-el-Fitr neno la Kiarabu linalomaanisha "sherehe za kufunguwa" kawaida huadhimishwa kwa siku nne katika maeneo mengi yaliyo na Waislamu wengi duniani, ambapo watu hujikusanya pamoja kwa ajili ya chakula, sala na michezo, hasa kwa watoto.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga