Waislamu wa EU wana imani na demokrasia, ubaguzi ukiongezeka
22 Septemba 2017Kulingana na utafiti huo uliofanywa kwa waislamu 10,500, ni kwamba Waislamu walioko Ulaya wana imani kubwa na taasisi za kidemokrasia kuliko wananchi kwa ujumla, japo wengi wao wanahisi kubaguliwa kwasababu ya dini yao, Utafiti huo uliochapishwa na Shirika la umoja wa ulaya linalohusika na haki za msingi lililoko Vienna FRA umeonyesha kwamba asilimia 76 ya waislamu wa Ulaya wanahisi kwamba ni sehemu ya jamii ya nchi wanazoishi, wakati sehemu kubwa ya waislamu wanapinga vurugu.
Shirika la FRA ilifanya utafiti huu miongoni mwa wahamiaji na kizazi cha pili cha wahamiaji kutoka Uturuki, Afrika na Asia katika mataifa 15 ambayo ni wanachama wa umoja wa ulaya.
Kulingana na mkurugenzi wa FRA Michael O'Flaherty, matokeo haya ya uchunguzi yanakinzana na madai ya kuwa waislamu hawajaunganishwa katika jamii zetu. Alisema, "hata hivyo, kwamba Waislamu ambao wanabaguliwa au ambao ni waathirika wa uhalifu wa chuki wanahisi hawana mafungamano na jamii zao."
Ni asilimia 68 tu ya waliohojiwa wanaohisi kuathirika na ubaguzi na walisema kuwa mafungamano na nchi zao ni imara ikilinganishwa na asilimia 81 ambao hawakuwa na uzoefu huo mbaya. Matokeo yanaonyesha kwamba ubaguzi unaongezeka.
Karibu mmoja kati ya watano waliohojiwa walisema kuwa wamebaguliwa na wamiliki wa nyumba, waajiri au viongozi wa umma katika miaka mitano iliyopita kwa sababu ya dini yao. Katika utafiti wa 2008, idadi ilikuwa moja tu katika 10. Kutengwa kwa watu ni tofauti kati ya nchi za umoja wa ulaya. Waafrika walihisi kubaguliwa zaidi nchini Ujerumani, Uholanzi na Denmark, huku waturuki wakihisi kubaguliwa Uholanzi na nchini Ugiriki.
Huku kukiwa na mijadala ya umma juu ya viwango vya uhalifu kati ya wageni na mashambulizi ya kidini, watafiti waliwauliza waislamu kama itakuwa sawa kutumia vurugu katika kukabiliana na matusi ya dini au ya kikabila.
Zaidi ya asilimia 85 walisema vurugu haikubaliki katika visa hivyo,wakati karibu asilimia 10 walisema inakubalika katika hali fulani.Wahamiaji wasiokuwa waislamu wanapendelea kujiepusha zaidi na vurugu.
Waislamu wanahesabika kuwa asilimia nne ya idadi ya watu katika Umoja wa ulaya.
Utafiti huu ulifanyika mwaka jana kati ya wakazi wa muda mrefu katika umoja wa ulaya isipokuwa wale ambao wamefika tangu kuongezeka kwa wakimbizi mwaka 2015. Nchi nyingi wanachama zina mikakati ya serikali ya kuwajumuisha wageni, na wengi wanatarajia wahamiaji kukabiliana na mazingira mapya, lakini ripoti hiyo inasema wahamiaji hawapati fursa kubwa ya kushiriki katika jamii.
Shirika la FRA limesema kuwa wahamiaji wangeweza kukuza mizizi yao barani ulaya iwapo mamlaka husika zitakusanya maoni yao kabla ya kuendeleza sera. Kwa namna fulani, waislamu wameonekana kuwa watu walio na uwazi zaidi kuliko wazungu wa kawaida, utafiti umeonyesha. Wakati asilimia 30 ya wananchi wa Umoja wa ulaya wakisema watakuwa na wasiwasi ikiwa mtoto wao alikuwa na uhusiano na muislamu, asilimia 17 pekee ya waislamu wana shida na ndoa za dini tofauti.
Mwandishi: Fathiya Omar
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman