1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu Ulaya: Msaada wa huduma ya simu kwa vijana wa Kiislam Uingereza

Admin.WagnerD14 Oktoba 2010

Vijana wa Kiislam wa nchini Uingereza wanasita kuomba msaada kutoka vyombo vya serikali wakihofia kutokueleweka na katika kukabiliana na tatizo hilo, imetengenezwa huduma mpya ya simu inayoitwa The Muslim Youth Helpline

https://p.dw.com/p/PeU8
Waislamu Barani Ulaya
Waislamu Barani UlayaPicha: picture alliance/dpa

Huduma hii ya Simu kwa Vijana wa Kiislam ni ya bure na ya siri, ambayo kijana anaweza kuitumia kuzungumzia masuala anayokabiliana nayo. Jumuiya inayoendesha huduma hii inategemea wataalamu wa kujitolea na ilianzishwa miaka kumi nyuma na vijana wanne wa Kiislamu, baada ya kuona kuwa familia na marafiki zao hawana wa kumkibilia kumuomba msaada wanapokuwa na matatizo.

Kiongozi wa Jumuiya hii, Bi Akeela Ahmed, anasema mfumo wa serikali wa ushauri huwa unayaangalia masuala yanayohusiana na imani na kitamaduni kijuujuu. Masuala hayo ni kama vile ndoa za kulazimishwa na udhalilishaji wa kijinsia. Kutafuta ushauri wa masuala haya kutoka viongozi wa kijamii nako pia huweza kuzusha matatizo zaidi kwa vijana wa Kiislam wanaotafuta sikio la kuwasikiliza.

Taswira ya Uislam nchini Ujerumani
Taswira ya Uislam nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

"Walipojaribu kutafuta msaada katika kiwango cha jamii juu ya masuala kama vile mfadhaiko au matumizi ya madawa ya kulevya, walikumbana na ukosefu wa uelewa au mtazamo kwamba haya si mambo ya kuzungumzwa, nao wanayasukumiza chini ya zulia. Hata wanapojaribu kuigeukia serikali kutaka msaada, nako pia wapata majibu ambayo kwa kweli hayatambui mahitaji yao." Anasema Bi Akeela.

Kwa kawaida hii, huduma hii ya simu ya kutoa msaada hupokea malalamiko kutoka kwa vijana na mabarobaro, lakini imewahi pia kupokea vilio vya watoto hadi wenye umri wa miaka mitano au hata wazee wanaolalamikia vitendo vya watoto wao.

Akeela Ahmed anasisitiza kwamba matatizo yanayowakumba sio yale yanayowahusu wao kama Waislam tu, bali kama wanaadamu wa kawaida.

Hata hivyo, huduma hii ya simu ya ushauri nasaha kwa vijana wa Kiislam inakosolewa na wengine kwamba ni huduma inayojishughulisha na kundi dogo tu la vijana wa Kiislam ambao wanajitambulisha kwa Uislam wa imani tu. Mwenyekiti na mwasisi wa taasisi ya FATIMA inayojihusisha na utetezi wa wanawake na familia zao, Parvin Ali, anahofia kwamba vijana wa Kiislam wanageukia huduma inayoitwa ya Kiislam wakitarajia kusikia ujumbe wa Kiislam na hivyo hawawezi kupata mawazo nje ya mfumo wao wa maisha.

"Waislamu ni wepesi wa kusema kile wanachokitaka kutoka kwa wasio Waislam, lakini ni wagumu wa kutoa. Halijawahi kuwa jambo la nipa-nikupe. Kila siku imekuwa 'tuache sisi tujichanganye na wewe, lakini wenyewe hawakubali kwamba wanapaswa kuufahamu utamaduni wanaoishi nao na kuona ni jambo lipi ambalo na wao lazima watoe kwa utamaduni huo."

Anasema Bi Parvin, akisisitiza kwamba, baadhi ya jamii hawaziamini sana taasisi za jamii zao wenyewe kwani wanadhani kwamba siri zao zinaweza kuwekwa wazi. Watu wanaogopa kwenda katika huduma kama hizi, kwa mfano kusema kuwa mmoja kati ya wanafamilia amejiingiza kwenye mirengo ya siasa kali, kwani siri hiyo inaweza kutoka na hivyo kuiathiri familia hiyo.

Lakini mwenyekiti wa Huduma ya Simu kwa Vijana wa Kiislam wa Uingereza, Akeela Ahmed, anasisitiza kwamba kutunza siri ni msingi muhimu wa jumuiya yake, na jumuiya yake inaamini inapotokezea mpigaji simu anatishia maisha basi mamlaka husika zinaarifiwa.

"Nina hakika kuwa kila raia atakubaliana na mimi kwamba ikiwa mtu anakutishia maisha, basi ni lazima uweke taarifa kwenye mamlaka za dola, ila kwa sasa hatujawa na taarifa za watu kuelemea kwenye siasa kali."

Huku pande zote zikikubaliana kwamba huduma kama hii ni muhimu katika kuwafanya Waislam wakubalike katika jamii za Ulaya, suala ni ikiwa kazi zake zingelikuwa na ufanisi kama zisingelikuwa kwa ajili ya Waislam na zinazoendeshwa na Waislam tu.

Mwandishi: Mohamed Khelef/Potts, Nina-Maria (DW-Englisch)

Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman