Waislamu milioni 1.5 waanza ibada ya hijja Saudi Arabia
10 Septemba 2016Ibada ya Hijja ya kila mwaka inayotekelezwa na Waislamu imeanza Jumamosi (10.09.2016) nchini Saudi Arabia huku hatua kali za kiusalama zikiwa zimeimarishwa kwa takriban mahujaji milioni 1.5 wanaoshiriki hija hiyo.
Baada ya kufanyika kwa taratibu za awali za ibada hiyo katika Msikiti Mkuu katika mji wa Mecca eneo takatifu kabisa kwa Waislamu duniani mahujaji hao Jumamosi wameanza kuelekea eneo la tambarare la Mina lilioko kama kilomita tano mashariki ya Meccca kwa kutumia vyombo mbali mbali vya usafiri na hata kwa miguu chini ya hali ya joto inayopindukia nyuzi joto 40.
Mahujaji hao watakuwa wanafuata nyayo za Mtume Muhammad (SAW) aliyefanya utaratibu huo huo wa ibada miaka 1,400 iliopita.Mamia kwa maelfu ya mahujaji wakiwa katika mavazi yao meupe yasiokuwa na mishono walianza kuondoka mji mtakatifu wa Mecca Jumamosi alfajiri kwa safari yao hiyo ya Mina ambapo watalala huko na watakamilisha hijja kwa kwenda kusimama kwenye mlima Arafat hapo Jumapili.
Tarehe 24 Septemba mwaka jana Mina palikuwa ndio mahala kulikotokea maafa mabaya kabisa katika historia ya hija kutokana na mkanyagano wakati mahujaji walipokuwa wakielekea kwenye Daraja la Jabarat kwa ajili ya kumpiga mawe shetani. Mwaka huu kumpiga mawe shetani kutaanza Jumatatu.
Usalama waimarishwa
Juu ya kwamba serikali ya Saudi Arabia imeendelea kusisitiza kwamba idadi ya watu waliokufa katika mkanyagano huo walikuwa 769 data kutoka maafisa wa nchi za kigeni kutoka zaidi ya nchi 30 wametowa idadi mara tatu zaidi ya hiyo kwamba waliokufa ni 2,297.
Saudi Arabia ilitangaza uchunguzi wa makanyagano huo lakini matokeo katu hayakuwahi kutangazwa.Safari hii hatua kadhaa za kuimarisha usalama zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na mahujaji kuvalishwa vibangili vya elektroniki vitakavyowasaidia kuwatambulisha wakati wa msongamano.Vibangili hivyo vitahifadhi data zao binafsi baada ya maafisa wa nchi za kigeni kuelezea wasi wasi wao juu ugumu wa kuwatambuwa mahujaji waliokufa kutokana na mkanyagano.Hatua hizo za usalama zinajumuisha pia uwekaji wa mamia ya kamera za uchunguzi katika maeneo takatifu.
Maelfu ya wananchi wa Iran hawakuweza kuhudhuria hijja ya mwaka huu kutokana na mvutano wa mrefu kati ya mataifa hayo ambapo Iran ina waumini wengi wa madhehebu ya Shia na Saudi Arabia linalodhibitiwa na Waislamu wa madhebu ya Sunni ambao ndio walio wengi nchini humo na mvutano wao ulizidi kupaliliwa kutokana na mkanyagano wa mwaka jana.
Wairan wakosa hijja
Licha ya hatua ambazo Saudi Arabia inasema imezichukuwa ili kuzuwiya msongamano na kuboresha usalama, serikali ya Iran inaendelea kuhoji haki ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kusimamia maeneo hayo takatifu kabisa kwa Waislamu.Nchi hizo hazina uhusiano wa kibalozi na zinahitilafiana juu ya masuala kadhaa ya kanda vikiwemo vita vya Yemen na Syria .
Iran ndio iliopoteza mahujaji wengi katika mkanyagano wa mwaka jana ambao wanatajwa kufikia 464 na kwa mara ya kwanza haiukutuma mahujaji wake mwaka huu baada ya miongo mingi baada ya nchi hizo kushindwa kukubaliana juu ya masuala ya usalama na vifaa.Maelfu ya watu nchini Iran hapo Ijumaa waliandamana kupinga kutokuwepo kwa nchi yao katika ibaada hii ya hijja.
Takriban Waislamu milioni 1.3 kutoka takriban nchi 160 wako nchini Saudi Arabia mahala ulikozaliwa Uislamu kwa ajili ya ibada ya hijja ya mwaka huu ikiwa ni ziada ya mahujaji wa ndani ya nchi 102,000.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa
Mhariri :Gakuba Daniel