1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wairaq waanzisha vuguvugu la kupambana na kundi la al-Qaeda.

Sekione Kitojo4 Oktoba 2007

Wairaq kwa maelfu wanajitokeza kujiunga na majeshi ya usalama nchini humo katika mapambano dhidi ya kundi la al-Qaeda kama sehemu ya hatua za uamsho zilizoanzia katika jimbo la Anbar.

https://p.dw.com/p/C7in

Kauli mbiu ya hivi sasa katika nchi hii iliyoharibiwa kwa vita ni pamoja na maridhiano, raia wakereketwa, ulinzi wa raia katika maeneo wanayoishi, na malipo. Juhudi ni pamoja na viongozi wenye ushawishi mkubwa wa kikabila wanaojiunga pamoja kuwawinda wenye imani kali hadi mipango ya maeneo ambapo watu wanaojitolea wakivaa mshipi wa rangi ya machungwa na wakiwa na bunduki za AK 47 wanawapa taarifa polisi juu ya shughuli zinazotiliwa mashaka ama kuwakamata watuhumiwa.

Kwa idadi ya hivi karibuni , kwa mujibu wa kamanda wa jeshi la Marekani , kanali Robert Menti , kiasi cha Wairaq 50,000 nchini humo wamejiunga na juhudi tofauti 150, 25 zikiwa mjini Baghdad, zenye lengo la kupambana na wapiganaji na kurejesha hali ya kawaida ya utulivu katika maeneo waishimo raia.

Ni juhudi za kukataa imani kali , amesema kanali Menti, ambaye ni naibu mkuu wa kitengo cha jeshi la Marekani cha maridhiano nchini Iraq. Ni hali ya mabadiliko yanayofanywa na raia wa Iraq, wakiwa ni Washia na Wasunni, ambao wamechoshwa na vita.

Baadhi wanajitokeza kutokana na malipo yanayotolewa, kiasi cha dola kumi kwa siku, katika baadhi ya nyakati huvutiwa na sare za jeshi zinazotolewa, na katika baadhi ya nyakati watu huvutiwa na fulana T-Shirt, gunia la chakula ama malipo ya jumla ya dola 150.

Hatua hiyo ilianzishwa na Sheikh Abdul Sattar Abu Reesha, kiongozi wa kikabila kutoka madhehebu ya Sunni katika jimbo la magharibi la Anbar, ambaye Septemba 14 mwaka jana aliunda ushirika wenye nguvu wa makabila 42 unaojulikana kama umoja wa uamsho wa Anbar. Kundi hilo limeahidi kupambana na wapiganaji wa al-Qaeda kwa kuunda vikundi vyao vya ulinzi na kuwapeleka wanamgambo wao katika jeshi la polisi la maeneo hayo. Abu Reesha aliuwawa kwa bomu lililotegwa kando ya barabara Septemba 13, siku moja baada ya kufikia mwaka wa kwanza wa kuundwa kwa kundi lake hilo, katika shambulio katika mji mkuu wa jimbo la Anbar wa Ramadi , shambulio ambalo baadaye kundi la al-Qaeda lilidai kuhusika.

Brigadia Jenerali Mark Gurganus, kamanda ambaye anafanyakazi katika jimbo la Anbar, amesema kuwa licha ya kifo cha Abu Reesha , kazi ya baraza la uamsho la Anbar zinaendelea, likiongozwa na mdogo wake Sheikh Reesha , Ahmed.

Makundi ya uamsho kama lile lililoanzishwa na Abu reesha yameanzishwa katika jimbo la kaskazini la Salaheddin na wilaya ya Al-multaqa karibu na mji wa kaskazini unaopatikana visima vya mafuta wa Kirkuk.

Majeshi yetu yanafanyakazi kwa uratibu na wizara ya ulinzi na wizara ya mambo ya ndani na yamefanya zaidi ya mapambano 100 dhidi ya al-Qaeda , amesema Sheikh Sabah Mutashar al-Shimmary, kiongozi wa baraza la uamsho la Salaheddin.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki ameonyesha wasi wasi wake , iwapo kampuni binafsi la ulinzi la Marekani Blackwater linaweza tena kuwa na nafasi ya kufanyakazi nchini Iraq hapo baadaye kwasababu ya idadi kubwa ya matukio ya kupigana risasi ambayo kampuni hilo limehusika nayo.