Wahouthi wampa changamoto Rais wa Yemen
21 Januari 2015Akizungumza masaa machache baada ya wapiganaji wake kuonyesha nguvu zake kiongozi wa Wahouthi Abdel Malek al-Houthi amemuonya Rais Abd-Rabbu Mansour Hadi kwamba inabidi atekeleze makubaliano ya kushirikiana madaraka yaliofikiwa wakati wapiganaji wake waliponyakuwa mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa hapo mwezi wa Septemba.
Akizungumza moja kwa moja kwa njia ya televisheni amemtaka rais huyo wa Yemen kuyatekeleza makubaliano hayo kwa faida yake na kwa faida ya wananchi kwa jumla.
Houthi anayathamini makubaliano hayo kutokana na kwamba yanalipa kundi lake la madhehebu ya Shia ushiriki katika asasi zote za kijeshi na kiraia za taifa.Kundi hilo linaonekana kuwa mshirika wa Iran katika mapambano yake ya kuwania ushawishi na Saudi Arabia katika kanda hiyo.
Hadi aungwa mkono na jumuiya ya kimataifa
Rais Hadi ambaye ni mshirika wa mataifa ya magharibi na mwenye kuunga mkono kwa nguvu mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani za Marekani dhidi ya wapiganaji wa kundi la Al Qaeda nchini Yemen amekuwa akizidi kutofautiana na Houthi kuhusu rasimu ya katiba inayokusudia kukomesha mzozo wa miongo kadhaa na maendeleo duni nchini humo.
Kuibuka kwa Wahouthi hapo mwezi wa Septemba kama kundi lenye nguvu nchini Yemen kwa sasa kumetibua mvutano katika fani nzima ya kisiasa nchini Yemen na kuzidisha hofu kwa nchi hiyo kuzama zaidi kwenye dimbwi la ukosefu wa utulivu katika nchi ambayo kuna matawi mengi ya Al Qaeda yenye harakati kubwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtaifa Ban Ki- moon amelaani matumizi ya nguvu yanoendelea nchini humo na kutaka utulivu urudishwe nchini humo.
Jumuiya ya Kimataifa imeendelea kumuunga mkono Rais Hadi.Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi yaliofanywa jana na Wahuthi na kuidhibiti Ikulu ya Rais.
Iran yaunga mkono uasi
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Marekani taarifa za karibuni kutoka Sanaa zimedokeza kwamba waasi wa Houthi wameyazingira makaazi binafsi ya Rais Hadi na kwamba wako karibu na kudhibiti makao yake rasmi au tayari wameyadhibiti.
Marekani imesema Iran inaunga mkono uasi huo wa Wahuthi kwa msaada wa kifedha na wa kisiasa.Inasemekana kwamba serikali za kigeni zimegunduwa shehena ya silaha ikisafirishwa kutoka Iran kwenda kwa waasi hao wa Kihouthi.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Ghuba leo wanatazamiwa kujadili mzozo huo wa Yemen katika mkutano wa dharura utakaofanyika katika mji mkuu wa Saudi Arabia Riyadh.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri : Iddi Ssessanga