Wahouthi wako tayari kusimamisha vita
16 Novemba 2016Tangazo hilo la Jumatano (16.11.2016) linaonekana kuthibitisha taarifa za makubaliano yaliofafanuliwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry siku moja kabla ambapo amesema yanajumuisha usitishaji wa mapigano utakaoanza hapo Alhamisi.
Mohammed al- Bukhaiti mjumbe wa baraza la kisiasa la kundi la Ansarullah la Wahouthi amesema Saudi Arabia pia imekubali kumaliza kujiingiza kwake katika vita hivyo juu ya kwamba hakuna uthibitisho rasmi kutoka Saudi Arabia.
Muungano wa nchi za Kiarabu ulijiingiza katika mzozo huo wa Yemen hapo mwezi wa Machi mwaka jana kumuunga mkono Rais Abd- Rabbu Mansour Hadi baada ya Wahouthi waliokuwa wakiungwa mkono na Iran kuukaribia mji mkuu wa muda Aden na kumlazimisha kiongozi huyo akimbilie uhamishoni nchini Saudi Arabia.
Msimamo wa Wahouthi
Bukhait ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba msimamo wa kundi la Ansarullah ulikuwa na bado uko pale pale kusimamisha vita hivyo na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayojumuisha pande zote za kisiasa.
Amesema kile kilicho kipya ni msimamo wa Saudi Arabia ambayo imekubali kusimamisha vita hivyo ikiwa ni mmojawapo wa wahusika wa mzozo huo.
Baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya mabomu na mapigano mengine hakuna upande ulioibuka kuwa mshindi katika vita hivyo vilivyowapotezea makaazi zaidi ya watu milioni tatu na kuwaacha baadhi ya wananchi kwenye ukingo wa kufa njaa pamoja na kuwapa upenyu tawi la al Qaeda kutanuwa operesheni zake.
Uhalifu wa kivita
Wataalamu na mashirika ya haki za binaadamu wanasema baadhi ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na Saudi Arabia ni sawa na uhalifu wa kivita.
Abdel Rashid al Faqeh kiongozi wa shirika la haki za binaadamu la Mawatwaa nchini Yemen anasema "Nafikiri kwamba Saudi Arabia hauishughilishwi na yanayojiri ni kama vile dunia imewapatia kibali cha kufanya wanavyotaka kwa kuwaambia hawa watu ni maskini na damu yao haina hasara kwa jukwaa kuu duniani na kwa namna dunia kwa jumla inavyowasiliana na Saudi Arabia."
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwa kile kinachooneka yumkini ndio ikawa safari yake ya mwisho huko Ghuba kabla ya kumalizika kwa muhula wa Obama hapo mwezi wa Januari amesema hapo jana mkutano wa maafisa kutoka kundi moja la Wahouthi na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umekubali kusitishwa kwa mapigano kuanzia Alhamisi (17.11.2016).
Ikionyesha ugumu wa hali iliyvo serikali ya Hadi kwa haraka iliikataa hatua hiyo kwa kulalamika kwamba imekiukwa.Nakala za mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa ambazo shirika la habari la Reuters liliweza kuzipata mwezi wa Oktoba zilidokeza kwamba kiongozi huyo atawekwa kando katika serikali yoyote ile mpya.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP
Mhariri :Gakuba Daniel