Wahouthi waadhimisha miaka mitatu ya kuteka Sanaa.
21 Septemba 2017Waasi Wahouthi na makundi yanayomuunga mkono aliyekuwa rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh waliuteka mji wa Sanaa mnamo tarehe 21 Septemba mwaka wa 2014 na kulitumbukiza taifa la Yemen katika machafuko na kushawishi muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati dhidi yao mwaka uliofuata.
Alhamisi, ndege za muungano huo ziliweza kusikika angani mwa Sanaa huku halaiki ya watu, waasi wahouthi na wasaidizi wa Saleh wakikusanyika katika uwanja wa Sabaeen mjini Sanaa, kulingana na mpiga picha wa shirika la habari la AFP. Uwanjani, maafisa wa usalama walikuwa chonjo kuimarisha usalama wakipekua magari vilivyo yanapoingia mji huo mkuu and kukaribia eneo hilo.
Kulikuwa na kila aina ya shamrashamra, utumbuizaji na hotuba. Akihutubia umati wa watu, mkuu wa serikali ya waasi Abdel Aziz Bin Habtoor, ameahidi kuokoa Wayemen wote. Amesema, "Hatuwezi kukubaliana juu ya ukombozi wa ardhi zetu."
Aliishtumu Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, mwanachama muhimu wa muungano kwa kuchukua nafasi ya maeneo ya kusini mwa Yemen na baadhi ya mikoa yake ya mashariki. Matamshi haya yanajiri wiki moja baada ya kiongozi wa waasi Abdul Malik Al Huthi kutishia kurusha makombora katika Umoja wa Falme za Kiarabu na kuvishambulia vifaru vya Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu.
Siasa za Yemen
Miaka mitatu iliyopita hadi leo, wahouthi waliudhibiti mji wa Sanaa pamoja na makao makuu ya serikali na maeneo ya kijeshi kwa msaada wa vikosi vinavyomuunga mkono rais wa zamani Saleh. Mnamo Januari 2015 walimkandamiza Rais Abedrabbo Mansour Hadi na kumfanya kukimbia mji wa pili wa Yemen, Aden, ambaye baadaye aliutangaza kuwa mji mkuu wa muda mfupi.
Mnamo Machi mwaka huo muungano uliokuwa ukiongozwa na Saudi Arabia ulianza kampeni yake ya kijeshi kuwashambulia wahouthi na kumrejesha Hadi mamlakani. Vita vilivyopo nchini Yemen vimewaua watu zaidi ya 8,500 na kuwajeruhi karibu 49,000, kulingana na shirika la afya duniani, WHO.
Zaidi ya Wayemen millioni 17 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na janga la taifa la kipindupindu limeua zaidi ya watu 2,100 tangu Aprili. Taifa la Yemen leo limegawanyika pande mbili, ambapo kambi ya wa Huthi na Saleh ikidhibiti eneo la kaskazini na muungano unaounga vikosi vya serikali wanaopambana na wahuthii pamoja na wale wenye itikadi kali ikiwa ni pamoja na Al Qaeda wakidhibiti kusini. Mji mkuu wa sanaa unadhibitiwa na wahuthi na vikosi vinavyomuunga mkono rais wa zamani. Saleh aliitawala Yemen kwa zaidi ya miongo mitatu kabla ya kujiuzulu mwaka wa 2012 baada ya kipindi kirefu cha umwagikaji damu kushuhudiwa.
Taifa hilo limeendelea kushuhudia vita vikali vya kisiasa lakini Aprili Longley Alley, mchambuzi wa masuala ya Yemeni katika Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na majanga, alisema Wahuthi na Saleh wangeweza kudumisha uhusiano wao kwa muda mrefu kama vita vitaendelea. "Tofauti za kiuchumi na za kisiasa kati yao zimepungua lakini pia wanajua kuwa mgawanyiko wa kijeshi utawanufaisha maadui zao," aliliambia shirika la habari la AFP.
Mvutano wa hivi karibuni kati ya Wahuthi na Saleh unaweza, hata hivyo, kutoa fursa ya mazungumzo, alisema.
"Saudi Arabia, pamoja na Kuwait na Oman, zinapaswa kuita pande zote mbili za Yemeni kwenye meza ya mazungumzo," Alley alisema. Vinginevyo, alisema, "Al-Qaeda walioko kwenye eneo la bahari ya bara Arabu na kikundi kidogo cha wapiganaji wa silaha ambacho kinashirikisha vikundi mbalimbali vya mapigano ndio wataonekana wazi kuwa washindi."
Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE
Mhariri:Josephat Charo