Wahariri wanatoa maoni juu ya kuuawa kwa Bin-Laden
4 Mei 2011Gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linazingatia suala la uadilifu kuhusiana na jinsi Osama Bin- Laden alivyouawa.
Mhariri wa gazeti hilo anasema ni kweli kwamba Bin Laden alikuwa gaidi aliesababisha vifo vya maalfu ya watu ambao hawakuwa na hatia.Mhariri huyo pia anasema ,kwa jumla watu wengi duniani wanakubaliana kwamba ,ilikuwa sahihi kumzima Bin Laden.Lakini anakumbusha kwamba pia pana sheria za kimataifa, kwani sasa Marekani inafanya bidii ili kuthibitisha kwamba halikuwa lengo lake kumuua Bin Laden katika nchi nyingine.
Mhariri wa Berliner Zeitung pia anasema, yumkini kifo cha Bin Laden kimeifanya Marekani, pawe mahala pazuri zaidi kwa Rais Obama. Hata hivyo mhariri huyo anaeleza kuwa Rais Obama ameshangiliwa sana ,kwa kile kinachoitwa uongozi thabiti baada ya Bin Laden kuuawa.
Lakini jinsi alivyouawa kumeleta madhara kwa mapinduzi yanayotokea katika nchi za kiarabu. Yeyote anaetaka haki na sheria anahitaji msaada na siyo kujichukulia sheria mkononi.!
Gazeti la Südkurier pia linatilia maanani kuwa Rais Obama anaendelea kukanusha kwamba alitumia siasa ya mabavu dhidi ya Bin Laden! Gazeti hilo linaeleza kuwa kuwa Ikulu ya Marekani inasisitiza kwamba lengo lilikuwa kumkamata Bin Laden na siyo kumuua. Lakini yapo maswali kadhaa: kwa mfano kwa nini mwili wa Bin Laden haukupelekwa Marekani ili kufanyiwa uchunguzi? Kwa nini mwili wake ulitoswa baharini? Na kwa nini picha juu ya jinsi alivyouawa hazijaonyeshwa?
Lakini mhariri wa gazeti la Westdeutsche anasema kifo cha Osama Bin Laden ni faraja kwa wengi. Mhariri huyo anaeleza kwamba Osama Bin Laden alikuwa mhalifu na muuaji,na ameondoka na maalfu ya roho za watu kifuani mwake. Hakuzikwa katika kaburi la kawaida ili kuepusha kumfanya shahidi, ambapo wafuasi wake wangelienda kusujudi.
Bin Laden asilani hastahili kuwekewa kumbukumbu! Kifo chake kimewafariji wengi,ila baadhi ya watu nchini Marekani wanasikitika kwamba hakufikishwa mbele ya mahakama kujibu mashtaka juu ya uhalifu alioutenda.
Gazeti la der Neue Tag limeandika juu ya mapatano ya kurejesha umoja wa wapalestina yaliyofikiwa baina ya Hamas na Fatah. Mhariri wa gazeti hilo anaitilia maanani kauli ya Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas, kwamba yeye peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumza na Israel. Mhariri huyo anasema kauli hiyo inaweza kusababisha mgongano baina ya chama cha Fatah na Hamas.
Mwandishi/Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/
Mhariri/ Abdul -Rahman