Wahariri wa Ujerumani waguswa na mauaji ya Ethiopia
19 Januari 2012Gazeti la Nordwest linauliza kwa nini watalii hao walienda katika sehemu ya hatari? Haja ya kujijuvya tamaduni za kigeni ni jambo linaloeweka,lakini haina maana mtu afanye uzembe!
Mhariri wa gazeti la Braunschweiger pia anauliza inakuaje mtalii anajipeleka katika sehemu ya hatari.? Mhariri wa gazeti hilo anawashauri watalii wapate habari za kutosha kabla ya kufanya safari.
Katika maoni yake gazeti la Märkische Allgemeine linakumbusha kwamba kwa muda wa miaka mingi wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imekuwa inatoa tahadhari kwa watalii juu ya hatari iliyopo katika jimbo la Afar, la kaskazini -mashariki mwa Ethiopia.
Anasema katika jimbo hilo kwenye mpaka baina ya Ethiopia na Eritrea wapo waasi wanaoendesha harakati kwa lengo la kujitenga na serikali. Kwa hivyo, kwa mashirika ya kitalii kuandaa safari kwa ajili ya wateja wao, za kuenda katika sehemu hiyo, ni uzembe.
Gazeti la Dresdner Neueste Nachrichten linasema katika maoni yake kuwa mkasa wa watalii watano kutoka Ulaya unaakisi hali halisi inayojiri nchini Ethiopia. Gaezeti hilo linafafanua kwa kusema Ethiopia ni nchi inayokabiliwa na baa la njaa mara kwa mara, ni nchi iliyomo katika harakati za kupambana na ugaidi nchini Somalia kwa ufadhili wa Marekani. Ethiopia pia inakabiliana kiadui na jirani yake , Eritrea.
Mhariri anatilia maanani kwamba Ethiopia inasikika katika vyombo vya habari pale ambapo raia wa Ulaya wanapohusika. Anasema mkasa wa watalii watano raia wa Ulaya unadhihirisha mazingira yanayowakabili watu katika eneo la pembe ya Afrika- yaani migogoro ya kikabila, vita, uharamia na mmomonyoko wa dola.
Mhariri wa gazeti la Badische anatoa maoni juu ya habari za kutia moyo nchini Ujerumani. Wakati sehemu ya kubwa ya bara la Ulaya inakabiliwa na mgogoro wa madeni, uchumi wa Ujerumani unatarajiwa kustawi mnamo mwaka huu vilevile. Juu ya habari hizo njema, Mhariri huyo anasema itachukua muda mrefu, na kwamba gharama kubwa zitahitajika ili kuutatua mgogoro wa madeni uliopo sasa barani Ulaya. Gazeti za Badische linasema huo utakuwa msingi wa ustawi unaowafiki na maslahi ya Ujerumani. Lakini Ujerumani itanufaika zaidi ikiwa nchi nyingine za Ulaya nazo pia zitainuka tena kiuchumi.
Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/
Mhariri/- Othman Miraji