1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri juu ya Obama na China

Abdu Said Mtullya7 Novemba 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya uchaguzi wa Marekani baada ya ushindi wa Obama na juu ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Kikomunsiti cha China.

https://p.dw.com/p/16eVg
Wamarekani wamchagua tena Obama
Wamarekani wamchagua tena ObamaPicha: dapd

Juu ya uchaguzi wa Marekani mhariri wa gazeti la "Landeszeitung Lüneburg" anasema haidhuru ni nani ameshinda uchaguzi na kuwa Rais wa 45 wa Marekani. Wamarekani wameamka na kuiona nchi yao ikiwa vile vile haijabadilika.Marekani bado ni nchi ile ile inayohamishia nje nafasi za ajira kana kwamba ni bidhaa. Mhariri wa "Landeszeitung Lüneburg" anasema Marekani bado ni nchi iliyogawanyika baina ya matabaka ya kihafidhina na ya kiliberali, na ukosefu wa maridhiano unatishia mkwamo ndani ya nchi na kushindwa katika sera za nje.

Mkutano Mkuu wa chama cha kikomunisti nchini China unaanza hapo kesho mjini Beijing. Gazeti la "Rhein-Necker"linatoa maoni yake juu ya mtu anaetarajiwa kuwa kiongozi mpya wa chama na dola, Xi Jingping.

Mhariri wa gazeti hilo anasema hakuna anaejua kitakacholetwa na XiJingping kwa wananchi wa China. Kinachojukulina ni ukweli kwamba kiongozi atakaemrithi,Hu Jintao aliruhusu kustawi kwa upendeleo na rushwa nchini.Kinachojulikana pia ni kwamba baadhi ya viongozi waliomtangulia Xi Jinping waliziruhusu familia zao kujilimbikizia utajiri mkubwa sana.

Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anasema miaka 10 iliyopita haikuisogeza China mbele.Hali hiyo imewapa mwanya watu fulani wa kujinufaisha. Mhariri huyo anafafanua kwa kueleza kwamba hali hiyo imewawezesha watu wa tabaka fulani kujitajirisha kutokana na kustawi kwa mfumo wa ubepari wa dola. Mfumo huo umewatajirisha watu fulani kwa gharama kubwa ya umma wa China. Kwa hiyo swali muhimu la kuuliza ni iwapo viongozi wapya watakuwa na ujasiri wa kuchukua hatua za kuleta mageuzi muhimu ya kisiasa na ya kiuchumi.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatoa maoni juu ya uhusiano baina ya Marekani na China. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba nchi mbili hizo ndizo zitakazoudhibiti ulimwengu katika miaka ijayo. Mhariri huyo anaeleza kuwa Marekani na China ni nchi mbili zitakazokuwa na dhima kubwa kabisa katika masuala ya kisiasa na kiuchumi duniani. Lakini kisimgi inafahamika kwamba misingi ya siasa zao inatafautiana. Licha ya mafanikio makubwa ya kiuchumi China haijabadilika kwa kiwango kikubwa. Nchi hiyo bado inatawaliwa katika msingi wa udikteta. Dunia inafuatilia kwa makini maendeleo ya China.

Hivi punde tu China itakuwa dola kuu la kiuchumi duniani. Na kwa hivyo dunia inatumai kwamba viongozi wapya watakaochaguliwa kwenye mkutano Mkuu wa chama cha kikomunisti wataifungua nchi yao kiuchumi na hivyo kuweza kuleta usasa wa kisiasa.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu