1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa mbabe Katanga kulipwa dola 250

24 Machi 2017

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imeagiza wahanga 297 wa mbabe wa zamani wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Germain Katanga, walipwe dola 250 kila mmoja kama fidia kutokana na uvamizi wa kijiji chao.

https://p.dw.com/p/2ZulB
Germain Katanga ICC Den Haag Urteil 23.05.2014
Mbabe wa zamani wa kivita DRC Germain KatangaPicha: picture-alliance/dpa

Uvamizi huo ulifanywa mwaka 2003, na huu ulipaji fidia ndio mpango wa kwanza kabisa wa ulipaji fidia wa mahakama hiyo.

Kutolewa kwa agizo hilo la fidia kunajiri baada ya Katanga kupewa kifungo cha miaka 12 jela mwaka 2014, kwa uhalifu uliofanywa katika kijiji cha Bogoro kilichoko eneo la Ituri huko DRC. Alishutumiwa kwa kusambaza silaha kwa jeshi lake katika shambulizi hilo, ambapo watu 200 waliuwawa kwa kupigwa risasi na kukatwa kwa panga.

Lakini shirika la kutetea haki za kibinadamu la National Observer for Human Rights nchini Congo, limeonesha kukerwa na kiwango hicho cha fidia.

Watetezi wa haki za kibinadamu wamelalamikia fidia hiyo kuwa ndogo

"Tunashukuru kwa hatua hiyo lakini tunaona pesa zenyewe ni kidogo sana, kutokana na usumbufu uliyotupata na hali ya kukiukwa haki za kibinadam," alisema naibu mwenyekiti wa shirika hilo Alexis Kanyenya, "watu waliopata shida kama ile hawawezi kufurahia, shida waliyopata haiwezi kulinganishwa na pesa kama hizo," aliongeza Kanyenya.

"Mahakama imeangazia na kukadiria fidia ya jumla ya wahanga 297 kuwa zaidi ya dola 3.7 na mahakama hii pia inaweka kiwango kinachostahili kutolewa na Katanga katika fidia hiyo kuwa dola milioni moja," alisema jaji aliyekuwa anaendesha kesi hiyo Marc Perrin de Brichambaut.

Niederlande Urteil Germain Katanga Internationaler Strafgerichtshof Den Haag Verteidiger
Mawakili wa Germain Katanga katika mahakama ya ICCPicha: Reuters

Jaji Brichambaut lakini aliongeza kusema, huenda Katanga aliyekuwa akifuatilia kesi hiyo kutoka jela moja mjini Kinshasa, akashindwa kutoa kiasi hicho cha pesa kutokana na kuwa kwa sasa hana nyumba wala mali. Jaji huyo alidai pia kiasi hicho cha dola 250 kwa kila mhanga wa bwana Katanga, sio malipo ya uhalifu mzima uliofanywa.

Mawakili walikuwa wamekadiria wateja wao walipata hasara ya zaidi ya dola milioni 16

Mahakama pia ilisema fidia ya jumla inastahili kuelekezwa katika miradi itakayowasaidia wahanga kupata makaazi, elimu na biashara zitakazowapatia mapato. Mfuko uliobuniwa chini ya mwongozo wa mahakama hiyo wa kuwasaidia wahanga, umetakiwa pia kutumia raslimali zake na utoe dola milioni moja, ili uwalipe fidia hiyo na ubuni mpango utakaowasilishwa mbele ya mahakama mwishoni mwa mwezi Juni.

Mfuko huo wa wahanga una akiba ya dola milioni 5 na dola milioni moja kati ya kiasi hicho, zimetengewa kesi ya mbabe mwengine wa kivita kutoka Congo, Thomas Lubanga, aliyehukumiwa miaka 14 jela mwaka 2012 kwa kusajili watoto katika jeshi nchini humo.

Kila mhanga aliyeathirika kisaikolojia kwa kifo cha mpendwa wake wa karibu ametakiwa kulipwa dola 8,000 na yule aliyempoteza mpendwa ambaye si wa karibu atalipwa dola 4,000.

Mawakili waliowawakilisha wahanga hao walikuwa wamekadiria hasara waliyopata wateja wao kuwa dola milioni 16.4, wakati walipoiwasilisha kesi hiyo mahakamani. Walikuwa wamepiga hesabu ya nyumba 228 kuchomwa moto kijijini humo, shule moja kuharibiwa na mifugo kutoweka au kuuwawa.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga