1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa kimbunga idai waendelea kupokea misaada

Admin.WagnerD26 Machi 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na misaada ya kiutu OCHA limearifu kwamba zaidi ya watu milioni 1.85 wamaethiriwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji pekee.

https://p.dw.com/p/3FfVi
Mosambik Idai Zyklon
Picha: Reuters/M. Hutchings

Mratibu wa OCHA Sebastian Rhodes Stampa amesema baadhi ya wahanga wa janga hilo wanakabiliwa na hali inayoweza kutishia maisha yao, wengine wakiwa wamepoteza mwelekeo wa maisha, lakini pia wakikabiliwa na athari zitakazoendelea kujitokeza taratibu.

Stampa, aliwaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba zaidi ya wafanyakazi 30 wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakielekea nchini humo wakati wengine wakija kwa kutumia barabara. Alisema, wanafungasha chakula na mahema na hii leo wataanza kuisambaza misaada hiyo kote nchini humo.

Waathiriwa hao tayari wameanza kupokea huduma za dharura kama za dawa, chakula na mahema wakati kina cha maji kikianza kupungua, huku shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu likionya kuhusu mripuko mbaya wa magonjwa kwenye eneo lililoathirika.

Mkuu wa shirikisho la mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC Elhadj As Sy alisema hapo jana kwamba wamekalia bomu linalotaka kuripuka, huku akitoa mwito wa juhudi mpya za kukabiliana na hali inayozidi kuzorota ya kiafya.

Waziri wa mazingira wa Msumbiji Celso Correia amewaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba shughuli za uokozi zinaendelea kuimarika, hasa baada ya baadhi ya barabara zilizoharibika kufunguliwa tena.

Harakati za kimataifa

Mosambik Hilfsgüter vom Roten Kreuz nach Zyklon Idai
Picha: Imago/Zuma/J. Hellin

Mjini New York, mkuu wa shirika la misaada Mark Lowcock amezindua mkakati wa kuisaidia Msumbiji kiasi cha Dola milioni 282 kuimarisha juhudi zinazoendelea nchini humo katika kipindi cha miezi mitatu. Lowcock, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kampeni kama hizo zitaendelezwa katika siku zijazo kwa ajili ya Zimbawe na Malawi.

Zaidi ya watu milioni 2 wameathirika na janga hilo nchini Msumbiji, Zimbabwe na Malawi ambako kimbunga Idai kilipiga na kusababisha mafuriko makubwa yaliyowafanya mamilioni ya watu kukosa makazi. Watu 700 wameripotiwa kuuawa katika mataifa ya Zimbabwe na Msumbiji, huku mamia wengine wakiwa hawajulikani walipo. 

Mwandishi: Harrison Mwilima/AFPE/RTRE

Mhariri: Gakuba, Daniel