Wahanga wa 'Holocaust' wakumbukwa
27 Januari 2017Mtawala huyo alipalilia fikra ya kuondokana na kile alichokiita udhaifu na uwoga miongoni mwa Wajerumani. Matokeo yake akasababisha kupotea kwa maisha ya ummati mkubwa wa watu ndani ya Ujerumani na katika nchi zilizokaliwa na wanazi. Lakini mauaji hayo yasingefikia idadi kubwa kama si kuhusika kwa madaktari, majaji, maafisa wa shughuli za utawala, wanasayansi na wengine.Palitumika kile kilichoitwa utafiti wa nasaba ambapo ilihusishwa sayansi na siasa. Maike Rotzoll , Naibu Mkurugenzi wa taasisi ya Historia na Maadili ya masuala ya Tiba ilioko katika mji wa Halle, ameiambia Deutsche Welle kwamba, maafisa wa utawala wa wanazi walijaribu kuzigeuza fikra zao kuwa ukweli wa kisiasa na kwa hakika walifanikiwa.
Hitler na wafuasi wake walianza kushinikiza ajenda yao mara tu baada ya kuingia madarakani Januari 30, 1933. Ilipofika mwezi Julai mwaka huo, Baraza la mawaziri la Hitler likapitisha sheria kuhusu vinasaba vya urathi. Sheria hiyo ikalifanya jambo la lazima kutolewa kizazi mtu yeyote aliyekuwa na uwezekano wa kupata watoto ambao watakua na athari kama za kiakili, mfadhaiko, uziwi, na hali nyengine za ulemavu . Mahakama za Ujerumani wakati huo zikawa zikitekeleza ushauri na mapendekezo ya madaktari na maafisa wa afya kwa jumla juu ya kuwaondolea uwezo wa kuzaa. Mahakama maalum za suala hilo, zikaidhinisha 90 asilimia ya matakwa ya aina hiyo na watu laki tatu hadi nne, wengo kutoka taasisi za magonjwa ya akili wakaondolewa uwezo wa kuzaa kabla ya vita vya vikuu vya pili vya Dunia. Wengine wakauawa baadae.
Kutoka kwenye kuondolewa uzazi hadi kuuwawa:
Mwezi Oktoba 1939, madaktari na wauguzi wakapewa amri kuwahamishia watoto wote wenye ulemavu na kasoro nyengine kiafya kwenye hospitali maalum ambazo ziligeuzwa kuwa maeneo ya kifo. Mpango huo uliongozwa na Philipp Bouhler, mkurugenzi wa ofisi ya binafsi ya hitler pamoja na Karl brandt mmoja wa madkatari binafsi wa Hitler. Mpango huo ukijulikana kama T-4 kifupisho cha mtaa ulioitwa Tiergartenstrasse nambari 4 mjini Berlin, mahala pa ofisi iliowaajiri na kuwalipa walioshiriki katika mauaji hayo.
Ilipofika 1940, kulikuwa tayari kuna vituo 6 vilivyoundwa katika sehemu tafauti za Ujerumani. watu 70,273 waliuwawa, wahanga walipewa sumu, waliwekwa na njaa hadi kufa pamoja na mpango huo wa T-4 kutumia vyumba vya mauaji kwa klutumia gesi, mpango uliotangulia mauaji katika kambi ya Auschwitz ba kambi nyengine za mauaji . Kwa mtazamo huo, mauaji hayo huchukuliwa kuwa maandalizi ya kile kilichowasibu wayahudi baadae yaani mauaji ya kimbari (Holocaust) .
Lawama na upinzani:
Watu zaidi ya 100,000 waliuwawa kama sehemu ya mpango wa T-4 ambao ulisitishwa Agosti 1941.Mauaji hayo yakasababisha malalamiko na upinzani hasa kutoka kwa Wakatoliki waliohisi yalikuwa kinyume na mafundisho ya dini yao. Kwa muda mrefu wan ahistoria waliandika kwamba hitler alilazimika kuufuta mpango huo kutokana na shinikizo la umma. lakini uvamizi wa Ujerumani nchini Urusi Juni 1941 ulimaanisha kuwa wengi miongoni mwa watekelezaji wa T-4 wakihitajika katika maeneo yaliokaliwa ya Ulaya Mashariki kwa ajili ya mpango mkubwa zaidi wa mauaji, na hasa katika maeneo yaliotekwa na Ujerumani ya Wanazi wakati wa vita. Wanahistoria wanataja idadi ya wahanga kuwa karibu 300,000. wauaji wakatumika kufanya kazi hiyo katika kambi za wafungwa za Sobibor na Treblinka.
Kumaliza Ukimya:
Kwa muda mrefu katika Ujerumani ya baada ya vita, waliuwawa kutokana na mpango wa mauaji walikuwa wahanga wa Wanazi waliosahauliwa. Familia zikisita kuwakumbuka jamaa zao waliokufa, huwenda ni kwa sababu ya aibu ya kushindwa kuwalinda, au kwa sababu ya ulemavu waliokuwa nayo baadhi yao wakiwemo wagonjwa wa akili. Lakini miaka baadae, Wajerumani- wanahistoria na wana dini- walianza kuibua kadhia za wahanga wa mauaji na maovu hayo.
Mwandishi Sigrid Falkstein kwa mfano, ambaye alizaliwa 1946, alishtushwa alipokuja kufahamu kwamba shangazi yake Anna Lehnkering aliuwawa katika kambi ya Grafeneck na hilo lilimpa ujasiri Falkstein kuandika kitabu kilichoitwa" Kumfuatilia Anna."
Aliiambia Deutsche Welle," Katika familia yangu hatukuwa tukizungumza kabisa kuhusu Shangazi yangu." Hivi sasa ninajua familia yangu ilikubwa na mchanganyiko wa mfadhaiko, ukimba na suala hilo kuwa mwiko." Kwa muda mrefu wahanga wote na walionusurika na familia zao- Magharibi na Mashariki mwa Ujerumani, walipigwa na hofu na mshtuko na kulazimika kunyamaza na kutodhukuru yaliotokea. Kwa upande mwengine kwa bahati mbaya, wengi wa wahusika katika ovu huo waliepuka kuadhibiwa na hivyo wakawa huru na kuendelea na shughuli zao.
Kuwapa heshima wahanga:
Falkenstein ambaye atazungumza katika bunge la Ujerumani katika hafla ya kuwakumbuka wahanga wa mpango wa mauaji mauaji wa Hitler wa walioonekana kutokuwa na faida katika jamii kutokana na ulemavu anasema, amepokea maelezo mengi ya kumpongeza kutoka kwa familia za wahanga ambazo zilipata moyo wa kutafuta ukweli kuhusu jamaa zao, baada ya kukisoma kitabu chake. Anasema,"Pengine nimeweza kutchangia kwa namna fulani kulifanya suala hili kufahamika kwa upana zaidi. Ni tukio la kishitoria, tukio la kukandamizwa haki, pengine tu kwa sababu wahanga walikuwa ni watu waliotazamwa kwa jicho jengine. Falkstein anasema kisa cha shangazi yake kinaonyesha kile kinachoweza kutokea pale tunapowaangalia watu kwa thamani na umuhimu wao na kuwatenga wengine kwa sababu tu ya mapungufu walio nayo -ulemavu katika miili yao. Hayo yalitangulia mauaji ya kimbari -mwanzo wa kile kinachojulikana kama Holocaust, ambapo jumla ya wayahudi milioni 6 waliuwawa.
Mwaka 2014, makumbusho maalum kuhusu wahanga wa T-4 ilifunguliwa katika mtaa wa Tiergarten nambari 4. Hafla ya kumbukumbu katika bunge la Ujerumani Bundestag, ni hatua moja mbele ya kuwapa heshima wahanga wa mpango wa mauaji wa Hitler na nafasi yao wanayostahiki katika historia.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Chase Jafferson
Mhariri:Yusuf Saumu
LINK: http://www.dw.com/a-37286088