1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji walioko katika meli ya Aquarius kugawanywa

Isaac Gamba
26 Septemba 2018

Wahamiaji 58 walioko katika meli ya uokozi ya Aquarius watapelekwa nchini Malta na baadaye kugawanywa katika mataifa ya Ufaransa, Ujerumani, Ureno na hatimaye Uhispania.

https://p.dw.com/p/35Vwq
Rettungsschiff Aquarius 2
Picha: Maud Veith/SOS Méditerranée

Waziri mkuu wa Malta Joseph Muscat ambaye sasa anahudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kuthibitisha hilo huku msemaji wa serikali akisema zoezi hilo litafanyika haraka ambapo wahamiaji hao watapelekwa kwanza Malta na baadaye kugawanywa katika nchi hizo nne.

Wahamiaji hao waliokolewa katika mwambao wa Libya na meli ya Aquarius inayohusika na shughuli za uokozi inayosimamiwa na shirika moja la kujitolea. 

Kwa mujibu wa shirika hilo miongoni mwa wahamiaji walioko ndani ya meli hiyo ni wanawake 17 na watoto wachanga 18 huku wengi wao wakiwa katika hali mbaya na wakionekana kuathirika kisaikolojia.

Ufaransa itawachukua wahamiaji 18 kati ya wale walioko katika meli hiyo, wakati Ujerumani na Ufaransa kila moja itawapokea wahamiaji 15 huku Ureno ikipokea wahamiaji 10, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka serikali ya Ufaransa kilipolieleza shirika la habari la AFP.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mbwa anayefahamika  kwa jina la Bella naye pia aliokolewa pamoja na wahamiaji hao katika kile kilichoelezwa ni mara ya kwanza kushuhudia mbwa kuokolewa katika mazingira ya aina hiyo.

Rettungsschiff Aquarius
Meli ya uwokozi ya AquariusPicha: picture-alliance/dpa/R. Runza

Meli hiyo ya Aquarius inaarifiwa ilikuwa ikielekea katika mji wa Marseille likiwa ni chaguo lake la mwisho baada ya serikali ya Italia inayofuata siasa kali za kizalendo kukataa meli hiyo kutia nanga katika moja ya bandari zake.

Hata hivyo, serikali ya Ufaransa imedokeza kuwa awali ilisita kuikaribisha meli hiyo ikisema ingepaswa kutia nanga katika bandari ya karibu iliyo salama iliyoko jirani na nchi inayokabiliwa na mgogoro ya Libya.

Kwa mujibu wa waziri mkuu wa Malta, tangazo hilo la nchi yake linakuja baada ya mazungumzo na serikali ya Ufaransa.

Meli hiyo ya Aquarius italazimika kwenda Marseille kuweka taratibu sawa kuhuu usajili wake baada ya serikali ya Panama kutangaza Jumamosi iliyopita itafuta usajili wa meli hiyo kufuatia malalamikoya Italia.

Mgogoro wa aina hiyo ulipatiwa ufumbuzi Agosti mwaka huu wakati nchi tano tofauti zilipokubali kuwachukua wahamiaji  aliokoloewa na meli ya Panama wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka kupitia bahari ya Mediterania.

Meli ya Aquarius nusura isababishe mgogoro wa kidiplomasia mwezi Juni wakati ilipokwama ikiwa na wahamiaji zaidi ya 600 baada ya Italia na Malta kukataa kuwapokea. 

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Agosti, wahamiaji 141 waliokuwa wamepanda meli ya Aquarius waligawanywa katika nchi za Ufaransa, Ujerumani, Luxembourg, Ureno na Uhispania.

Serikali ya Italia inasema ina wahamiaji wa kutosha  wanaowasili kwa njia ya boti, huku zaidi ya wahamiaji 70,000 wakiwasili katika fukwe za nchi hiyo tangu mwaka 2013.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef