1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wa Kisomali washambuliwa Yemen

17 Machi 2017

Boti moja iliyosheheni wahamiaji wa Kisomali imeshambuliwa nje ya ufukwe wa Yemen karibu na bahari ya Shamu na kuwauwa watu 31, wanawake na watoto miongoni mwao.

https://p.dw.com/p/2ZQYL
Mittelmeer Flüchtlingsboot
Wahamiaji wakivuka bahari ya ShamuPicha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Haya ni kulingana na shirika moja la Umoja wa Mataifa na afisa mmoja wa afya nchini Yemen.

Kulingana na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, watu hao walikuwa wamebeba stakabadhi za shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya wakimbizi UNHCR. Laurent De Boeck ni mkuu wa IOM na amesema shirika hilo linaamini kwamba watu wote waliokuwa kwenye boti hiyo iliyoshambuliwa walikuwa wakimbizi, lakini haijabainika wametokea sehemu gani ya Somalia.

Shirika la habari la SABA nchini Yemen linaloendeshwa na waasi wa Kishia, limesema shambulizi hilo lilifanywa na helikopta na lilifanyika katika ufukwe wa mkoa wa Hodeida, karibu na eneo la Bab al-Mandab. Shirika hilo la habari halijasema aliyehusika na shambulizi hilo.

Muungano wa majeshi umekuwa ukishambulia waasi wa Kishia Yemen

De Boeck ameongeza kwamba manusura 77 waliookolewa kutoka kwenye maji walipelekwa katika kituo cha uhifadhi cha Hodeida. Alisema IOM inawasiliana na hospitali, zahanati na hayo maeneo ya hifadhi ili itoe msaada unaohitajika wa kimatibabu.

Shiiten Jemen Houthis
Wapiganaji wa KihouthiPicha: picture-alliance/AP Photo/H.Mohammed

Mjini Geneva, msemaji wa IOM Joel Millman aliwaambia wanahabari kwamba hakuwa katika nafasi ya kuthibitisha iwapo helikopta ndiyo iliyohusika katika shambulizi hilo. "Uthibitisho wetu ni kwamba kuna vifo vingi na manusura wengi walioletwa hospitali," Millman aliliambia shirika la habari la Associated Press.

Muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukikabiliana na waasi wa Kishia nchini Yemen kwa takriban miaka miwili. Muungano huo wa majeshi umewashutumu waasi wa Kishia na Kihouthi kwa kutumia mkoa wa Hodeida kama njia ya kupitisha silaha kiharamu. Hakujakuwa na tamko rasmi kutoka kwa muungano huo wa majeshi.

Wahamiaji kutoka Afrika wanaoelekea Saudi Arabia hupitia Yemen

Waasi wa Kihouthi walichukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa na viunga vyake mwaka wa 2014, lakini mzozo huo umeenea tangu mwishoni mwa mwezi Machi 2015, pale Wahouthi walipoelekea katika mji wa kusini wa Aden na kuipelekea Saudi Arabia na marafiki zake wa Kisunni kuanza mashambulizi ya angani dhidi wa waasi hao wa Kishia.

Jemen regierungstreue Truppen erobern Provinzhauptstadt im Südjemen
Vifaru katika mji wa Lahj, Yemen kusini Picha: Getty Images/AFP/S. Al-Obeidi

Marekani pia ilifanya mashambulizi ya angani ikiwalenga wanachama wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Wahamiaji kutoka Afrika pia wamekuwa wakipitia nchini Yemen, wakiitumia njia hiyo kuelekea Saudi Arabia ambako wanatafuta kazi na maisha mazuri.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi UNHCR, limesema limesikitishwa na tukio hilo, ambalo linaonesha jinsi raia wasio na hatia wanavyoteseka kutokana na mzozo unaoendelea nchini Yemen.

Mwandishi: Jacob Safari/AP/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga