1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wadai kukatwa mishahara kunawaathiri

15 Agosti 2018

Wahamiaji wa kiafrika nchini Israel watishiwa kwamba watarejeshwa kwao na kukabiliwa na uhasama kutoka kwa wabunge na wakazi. Mbali na hayo wanakatwa asilimia ishirini ya mishahara yao.

https://p.dw.com/p/33DYH
Israel Protest gegen die Asylpolitik in Tel Aviv
Mamia ya wahamiaji walioingia Israel kupitia Misri Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Kuna takriban wahamiaji elfu 35 wa kiafrika na makundi ambayo yanawasaidia hivi karibuni yamesema kwamba sheria ya sasa, ambayo inairuhusu serikali kuchukua kiwango fulani cha mishahara yao kila mwaka na kuwarejeshea wakati tu watakapoondoka nchini humo, ni jaribio jingine la serikali ya Israel kuwalazimisha kuondoka.

Wahamiaji hao ambao wengi wanatokea katika mataifa ya Sudan na Eritrea, walianza kuingia Israel mwaka 2005 kupitia mpaka wa Misri, baada ya wanajeshi wa Misri kutibua kwa kutumia nguvu maandamano ya wakimbizi. Maelfu ya walivuka mpaka huo  na kupitia vizuizi hatari katika safari hiyo, kabla Israel kuukamilisha ukuta wa usalama mwaka 2012 ambao ulichangia wahamiaji hao kushindwa kuingia nchini humo.

Tangu mwaka huo taifa hio limekuwa likitafuta mbinu ya namna ya kuwashughulikia waliofanikiwa kuingia. Wengi wao walipata kazi ndogo ndogo katika mahoteli na mikahawa, huku wengine wakipata makazi katika mji wa Tel Aviv, ambapo wenyeji walianza kulalamikia kuongezeka kwa visa vya uhalifu.

Licha ya wahamiaji hao kudai kwamba wanatoroka vita katika nchi zao, serikali ya Israel inawaona kama watu tu wanaotafuta ajira na wanaotishia taswira ya taifa hilo. Mwezi Aprili, Israel ilitia saini makubaliano na Umoja wa Mataifa ili baadhi ya wahamiaji nchini humo waruhusiwe kuishi katika mataifa ya Magharibi, na wengine kusalia Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo Sabine Haddad amesema kwamba fedha zinazokatwa kutoka kwa mishahara yao zitawapa nafasi ya kuanza maisha upya watakapoondoka Israel. Haddad vile vile amesema, na hapa namnukuu,´´Kwa sasa serikali inshikilia Dola milioni 40 kutoka kwa zaidi ya wahamiaji elfu kumi na tatu. Miongoni mwa maelfu ambaye waliondoka hapa Israel kwa hiari, watu mia nne wamechukua fedha zao,´´mwisho wa kumnukuu.

Hata hivyo sheria hiyo imepingwa katika Mahakama Juu ya Israel, na wahamiaji wengi wanaichukuliwa kuwa mbinu nyingine ya serikali hiyo kuwashawishi waondoke kwa hiari. Baadhi yao wanasema licha ya kukabiliwa na wakati mgumu na uhasama, hawawezi kuondoka. Kulingana na sheria ya kimataifa, Israel hairuhusiwi kuwarejeha kwao wanaotafuta hifadhi nchini humo.

Mwandishi: Sophia Chinyezi

Mhariri: Mohammed Abdulrahman