Wahamiaji kutoka Afrika wamiminika Italia
28 Septemba 2009Kila mwaka maelfu ya wahamiaji, wengi wao wakiwa ni kutoka Afrika, wanamiminika kuja kufanya kazi kwa kipindi maalum nchini Italia, kama kuokota zabibu, mizeituni, nyanya na machungwa kwenye mashamba ya kusini mwa nchi hiyo. Wahamiaji hao ni wale wanaokwenda huko kutafuta kile wanachokiita maisha bora.
Mara nyingi wahamiaji hao huvumiliwa na maafisa wa nchi hiyo kwa sababu ya kazi yao wanayoifanya katika kuendeleza uchumi, kwani baada ya muda wa masaa mengi ya kazi hupatiwa ujira wa kuanzia euro 15 hadi 20 kwa siku na wahamiaji hao wanakaa kwenye kambi zisizo na maji wala umeme. Boubacar Bailo kutoka Guinea, anasema hakudhani kuwa maisha ya Italia yako namna hiyo. Bailo mwenye umri wa miaka 24, anayeishi katika eneo la Puglia linalolima asilimia 35 ya nyanya na linalojulikana kama ''Red Gold Triangle,'' anasema hata mbwa wanaishi maisha afadhali kuliko wao. Mhamiaji huyo kutoka Guinea anasema ni bora kufa kuliko kuishi maisha kama hayo, kwani mtu akifa huondokana na matatizo yote yanayomkabili.
Kwa mwaka huu mambo yamekuwa mabaya katika eneo la Puglia. Msukosuko wa uchumi umewalazimisha wenye kampuni za kaskazini mwa Italia kuzifunga kampuni hizo au kupunguza wafanyakazi, hivyo idadi ya wahamiaji wanaotafuta kazi imeongezeka katika eneo hilo na kufikia kiasi 2,000. Mwezi wa Septemba, mwaka huu, serikali ilitoa msamaha kwa wahamiaji haramu walioajiriwa kuwaangalia wazee wa Italia, lakini msamaha huo hauwahusu wale wanaofanya kazi katika mashamba ya nyaya. Bailo, ambaye amenyimwa hifadhi ya ukaazi na ambaye hana makaratasi ya Italia, amesema amefanya kazi siku nane katika miezi miwili iliyopita na hakupata hata euro 100.
Kasisi wa eneo hilo anayejaribu kuwasaidia wahamiaji, Padri Arcangelo Maira, anasema mfumo wa sasa wa utumwa ni kwa maslahi ya kiuchumi. Padri Maira anasema mwajiri anaweza kuwatumia wahamiaji na kisha akiwachoka anawafukuza kazi. Bailo anaishi pamoja na wahamiaji wenzake wapatao 600 ambao wengi wanatoka katika nchi za Afrika zilizokumbwa na vita, lakini hali halisi ya kambi yao ni mbaya. Lakini madaktari wasio na mipaka, (MSF), ambao tangu mwaka 2003 wamekuwa wakilifuatilia kwa karibu eneo hilo na kuwasaidia wahamiaji kupata mahitaji muhimu pamoja na huduma za afya, wanasema kitu zaidi kinatakiwa kufanywa ili kuwanusuru wahamiaji hao.
Daktari mmoja wa MSF, Alvise Benelli, anasema mazingira wanayoshi wahamiaji hao na sehemu wanazolia chakula ni hatari. Daktari huyo anasema vijana hao wadogo wanaoingia Italia wakiwa na nguvu, wanaumwa wakiwa katika eneo hilo, kwani wengi wao wanapata matatizo ya kuumwa mgongo na misuli kutokana na kupiga magoti au kuinama pindi wanapokuwa mashambani. Wahamiaji hao wanakuwa wamewasili nchini Italia baada ya kuzunguka nusu ya bara la Afrika na kunusurika katika safari za hatari za boti zinazoanzia safari zake nchini Libya.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)
Mhariri: Miraji Othman