1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 5,800 waokolewa kwenye pwani ya Libya

4 Mei 2015

Wahamiaji 5,800 wanaojaribu kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterenia, wameokolewa na walinzi wa pwani ya Italia, katika fukwe ya Libya ndani ya kipindi cha saa 48 zilizopita, huku maiti 10 zikiwa zimegunduliwa.

https://p.dw.com/p/1FJYm
Baadhi ya wahamiaji waliookolewa
Baadhi ya wahamiaji waliookolewaPicha: Picture-alliance/epa/Italian Coast Guard

Taarifa zinaeleza kuwa walinzi wa pwani ya Italia jana Jumapili waliwaokoa wahamiaji 2,150 waliokuwa wakijaribu kuingia Ulaya kutafuta maisha bora kwa kutumia boti zisizo salama katika Bahari ya Mediterenia. Wahamiaji wengine 3,700 waliokolewa siku ya Jumamosi na hivyo kuifanya idadi jumla ya wahamiaji waliookolewa mwishoni mwa juma lililopita kuwa 5,800.

Operesheni hiyo ya pamoja ya Umoja wa Ulaya kuwatafuta na kuwaokoa wahamiaji kwenye Bahari ya Mediterenia, inaendeshwa kwa kutumia meli mbili za walinzi wa pwani ya Italia, meli za jeshi la wanamaji wa Italia, meli ya Ufaransa inayofanya kazi kwa niaba ya shirika la ulinzi wa mipaka ya Ulaya-Frontex, meli inayomilikiwa na shirika la misaada kwa wahamiaji pamoja na madaktari wasio na mipaka-MSF.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya
Viongozi wa Umoja wa UlayaPicha: Reuters/E. Dunand

Jeshi la wanamaji la Italia limesema meli yake ya doria ya Bettica, imewaokoa zaidi ya wahamiaji 570 kutoka kwenye boti nne watu wanaokumbwa na shida baharini siku ya Jumapili, huku MSF ikisema meli yake ya MV Phoenix imewaokoa wahamiaji 369. Meli hizo zilizowaokoa wahamiaji hao zilikuwa zinaelekea kusini mwa Italia kwenye visiwa vya Lampedusa na Sicily.

Meli nyingine zakamatwa kwenye Pwani ya Libya

Wakati huo huo, jana walinzi wa pwani ya Libya wamefanikiwa kuzikamata meli kadhaa zilizobeba wahamiaji katika pwani ya Mediterenia na kuziamuru kurejea Libya katika mji wa pwani wa Misrata, ambao una kituo cha wahamiaji. Kanali Rida Issa, mlinzi wa pwani ya Misrata anasema wamezikamata boti tano zilizokuwa zimejaa zaidi ya wahamiaji haramu 500.

Shirika la habari la Ufaransa-AFP, limemnukuu afisa mwandamizi wa walinzi wa pwani ya Libya akisema wengi wa wahamiaji waliokuwa ndani ya boti hizo ni Waafrika. Mmoja wa wahamiaji kutoka Sudan ambaye ameokolewa, Nasim Ahmad amesema safari wanayosafiri ni ndefu na ngumu inayoweza kusababisha kifo, kwa sababu inachukua muda kusafiri kutoka Sudan hadi Ajdabiya na Ajdabiya hadi maeneo mengine yanayowafikisha hadi Tripoli.

Wahamiaji wakiwa kwenye meli waliyosafiria kuingia Ulaya
Wahamiaji wakiwa kwenye meli waliyosafiria kuingia UlayaPicha: picture-alliance/dpa/Garcia

Wakati huo huo, shirika la habari la Ujerumani-DPA, limewanukuu maafisa wa ulinzi katika pwani ya Ugiriki ambao wamesema kiasi ya wahamiaji 530 wamewasili kwenye visiwa kadhaa vya Ugiriki katika Bahari ya Aegen, njia inayotumiwa zaidi na watu wanaofanya biashara ya kuuza wahamiaji wanaoingia kwenye nchi za Umoja wa Ulaya.

Operesheni hiyo ya Umoja wa Ulaya Hatua inatokana na juhudi za umoja huo kuzuia vifo vya wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya kwa kuvuka Bahari ya Mediterenia. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuongeza juhudi zao, baada ya meli moja kuzama mwezi uliopita na kusababisha vifo vya karibu wahamiaji 800.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,DPAE,APE
Mhariri: Josephat Charo