1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina wa Merkel wawania kuibwaga SPD uchaguzi wa jimbo

14 Mei 2017

Muungano wa kihafidhina wa Kansela Angela Merkel unataraji kuibanduwa madarakani SPD kinachoongoza jimbo lenye idadi kubwa ya watu Ujerumani katika mtiihani wa mwisho wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa Septemba.

https://p.dw.com/p/2cwnW
Landtagswahl NRW Armin Laschet
Picha: Getty Images/L. Schulze

Kundi la muungano wa kihafidhina la Kansela Angela Merkel linataraji kukibanduwa madarakani chama cha SPD kinchoongoza jimbo lenye idadi kubwa ya watu nchini Ujerumani katika mtiihani wa mwisho wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi wa Septemba.

Katika uchaguzi huo wa Jumapili (14.05.2017) nchama cha Christian Demokrat (CDU) kinakusudia kitumia fursa ya ghadhabu ilioko miongoni mwa wakaazi milioni 18 wa jimbo la North Rhine- Westphalia kutokana na msongamano wa magari barabarani,kuongezeka kwa kiwango cha uhalifu na kudoofika kwa mfumo wa elimu pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kunyakuwa ushindi katika uchaguzi huo.

kwa mujibu wa maafisa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura inatajwa kuwa ni kubwa kuliko ile ya uchaguzi uliofanyika mara ya mwisho katika jimbo hilo.Katika masaa ya mwanzo ya kupiga kura hadi kufikia saa sita mchana asilimia 34 ya watu waliokuwa wanastahiki kupiga kura walikuwa tayari wameiga kura zao kwa kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2012. Vituo vya kupiga kura vitafungwa saa 12 jioni na makadirio ya kwanza yanatazamiwa kutolewa mara moja.

Chama cha SPD kimekuwa kiliongoza jimbo hilo la North Rhine-Wastphalia (NRW) takriban katika miaka yote ya kipindi cha baada ya kumalizika kwa vita tokea mwaka 1945 na kupoteza madaraka kwa kile inachokichukulia kama ni ngome yao kutazusha wasi wasi mkubwa kwa nafasi yao ya kuweza kumuangusha Merkel ikiwa imebakia miezi minne tu kabla ya kufayika uchaguzi mkuu nchini.

Matumaini ya kulinyakuwa jimbo

Landtagswahl NRW
Wapiga kura jimbo la North Rhine-Westphalia.Picha: Reuters/T. Schmuelgen

Ikiwa na asilimia 32 chama cha CDU kiko mbele kwa asilimia moja dhidi ya chama hicho cha SPD katika jimbo hilo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo na wana nafasi nzuri kuliko wapinzani wao ya kuunda serikali ya mseto na washirika wao wa jadi walioibuka upya chama cha kiliberali cha Free Demokrat.

Huo utakuwa ushindi wa tatu wa uchaguzi wa jimbo kwa wahafidhina ambao wametetea madaraka yao huko Saarland na kuindowa madarakani SPD katika jimbo la kaskazini la Schleswig -Holstein.Pia wahafidhina hao wamezidi kuwa mbele dhidi ya chama cha SPD katika ngazi ya taifa.

Kuungwa mkono kwa chama hicho cha SPD kuliongezeka hapo mwezi wa Januari wakati chama hicho kilipiomchaguwa spika wa zamani wa Bunge la Ulaya Martin Schulz kwa kiongozi wake na kuahidi kuimarisha huduma za ustawi wa jamii,kubadili mageuzi ya soko la ajira ambayo hayakuwa yakifurahiwa na ambayo yametanuwa sekta ya malipo ya chini Ujerumani.

Ujumbe wa Schulz wapoteza mvuto

NRW Wahlen Schulz gibt Stimme ab
Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz na mke wake wakipiga kura katika jimbo la North Rhine-Westphalia.Picha: Getty Images/L. Schulze

Lakini ujumbe wa Schulz wa kutaka kuwepo haki ya kijami umepoteza mvuto wake miongoni mwa wapiga kura kutokana na kuchelewa kufafanuwa mipango yake hiyo na itagharimu kiasi gani.Katika ngazi ya taifa chama cha SPD hivi sasa kiko nyuma ya chama cha CDU na chama ndugu cha Christian Socilal Union chenye makao yake huko Bavaria kwa kama asilimia 10.

SPD kimekuwa kikiongoza jimbo la North Rhine -Westphalia tokea mwaka 2010 kikiwa katika serikali ya mseto na chama cha Mazingira ambacho kuungwa kwake mkono kumedhoofika kwa zaidi ya nusu na kuwa na asilimia sita tu.

Itakuwa vigumu kwa chama cha SPD kufanikiwa kuunda tena serikali ya mseto  hususan kutokana na kwamba washirika wao wa kawaida chama cha Di Linke cha sera kali za mrengo wa kushoto nacho pia kina asilimia sita tu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa

Mhariri : Sudi Mnette