Wahafidhina na wasocial Democrats wataunda serikali
18 Oktoba 2013Mazungumzo hayo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu yanatarajiwa kudumu mwezi mmoja au miwili.Pande zote mbili zinaonyesha kuridhika na jinsi duru ya tatu ya mazungumzo ya kupima uwezekano wa kuunda serikali hiyo, ya tatu ya aina yake katika historia ya vyama hivyo,yalivyopita.
Alikuwa waziri mkuu wa jimbo la kusini la Bavaria Horst Seehofer aliyetangulia kutoa maoni yake aliposema:"Nimeridhika sana na nawatakia nyote wikiendi njema"
Hata kansela Angela Merkel ameonyesha kuridhika na jinsi mazungumzo hayo yalivyoendelea.
Badala yake mwenyekiti wa chama cha Social Democratic Sigmar Gabriel amesema wanaamini ufumbuzi wa maana kwa pande zote mbili utapatikana kuhusu masuala ambayo bado hayajatatuliwa.Sigmar Gabriel ameendelea kusema:"Hatukufika mbali hivyo kuweza kusema matukio thabiti yamepatikana wakati wa mazungumzo.Lakini tunaamini tunaweza kubuni msingi wa pamoja,pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU ili kuweza kukamilisha mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano kwa ufanisi."
Mkutano mkuu wa SPD jumapili
Wakuu wa chama cha SPD watakutana jumapili ijayo kwa mkutano maalum unaotarajiwa kutoa ridhaa ya kuendelezwa mazungumzo ya kuunda serikali pamoja na vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU/CSU.
Baadhi ya vigogo vya SPD,akiwemo pia waziri mkuu wa jimbo lenye wakaazi wengi zaidi la North Rhine Westfalia,bibi Hannelore Kraft,ambao awali walikuwa wakipinga kuundwa serikali ya muungano pamoja na CDU/CSU,wamebadilisha msimamo wao,
Maridhiano yasemekana yamefikiwa
Katibu mkuu wa chama cha kansela cha Christian Democratic Union,Herman Gröhe amesema anaamini,baada ya duru tatu za mazungumzo pamoja na Wasocial Democrats,kambi hizi mbili zinaweza kufikia maridhiano ya kutosha kuiongoza nchi kwa ufanisi."
Hadharani pande hizi mbili zinakwepa kutamka kwamba maridhiano yameweza kufikiwa hata hivyo duru za kuaminika
zinasema maridhiano yamefikiwa katika mada zilizokuwa zikizusha mabishano:SPD wamekubaliwa madai yao ya kuwepo kiwango cha chini cha mshahara kwa wote huku CDU/CSU wakifanikiwa kuzuwia mpango wa matajiri kutozwa kodi kubwa zaidi za mapato.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu